Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina, ametangaza mpango wa kufanya "mazungumzo ya kitaifa" na makundi mbalimbali Jumatano.
Waandamanaji vijana wameweka sharti la saa 48 kwa rais kuzingatia madai yao.
Jumatatu, Rajoelina alimteua Jenerali wa jeshi Ruphin Fortunat Zafisambo kuwa waziri mkuu mpya, wiki moja baada ya kuvunja baraza lake la mawaziri katika hatua iliyolenga kushughulikia malalamiko yaliyochochea maandamano ya Septemba 25.
Waandamanaji hao awali walijitokeza mitaani kupinga ukosefu wa maji na umeme nchini Madagascar. Sasa wanataka serikali kupambana na ufisadi na kuweka mikakati ya kutokomeza umasikini.
'Jamii inayojengwa juu ya mshikamano na kuheshimiana'
"Pamoja, lazima tuungane kupambana na maovu haya na kujenga jamii mpya inayojengwa juu ya mshikamano na kuheshimiana," alisema Rajoelina katika ujumbe wake Jumanne kwenye ukurasa wa Facebook wa ofisi yake.
"Kwa lengo hilo, mazungumzo na mashauriano ya kitaifa yatafanyika ili kusikiliza wasiwasi wa watu na kuandaa suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazotukumba."
Alisema mazungumzo hayo yaliyopangwa kufanyika Jumatano alasiri yatahudhuriwa na viongozi wa kiroho, wanafunzi, wawakilishi wa vijana, na wengine.