Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman kiongozi wa uhalifu wa kivita Darfur, Sudan
Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman kiongozi wa uhalifu wa kivita Darfur, Sudan
Mahakama ya ICC imempata Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman na hatia ya makosa 27 ya uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na ubakaji, mauaji na mateso katika jimbo la Darfur.
7 Oktoba 2025

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC Jumatatu ilimtia hatiani kiongozi wa kwanza wa wanamgambo kuwahi kufikishwa mahakamani kwa ukatili alioufanya katika jimbo la Darfur nchini Sudan zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Mahakama imempata Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman na hatia ya makosa 27 ya uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na ubakaji, mauaji na mateso.

Hukumu yake itaamuliwa baadaye baada ya duru mpya kusikilizwa. Lakini Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman ni nani?

Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman, anayejulikana pia kama Ali Kushayb, alikuwa mmoja wa viongozi wa Janjaweed, kundi linaloungwa mkono na serikali ambalo liliitikisa Darfur na kuua maelfu ya watu.

Uhalifu wa Abd-Al-Rahman ulifanyika wakati wa mzozo uliodumu kuanzia mwaka 2003 hadi 2020 na ulikuwa moja ya maafa makubwa zaidi ya kibinadamu duniani, na madai ya mauaji ya kikabila na kimbari dhidi ya wakazi wa eneo hilo.

Janjaweed waliwashambulia kwa utaratibu wanakijiji walioshutumiwa kuwaunga mkono waasi, na kusababisha shutuma za mauaji ya halaiki.

Sudan wakati huo iliongozwa na Omar El Bashir.

Umoja wa Mataifa unasema watu 300,000 waliuawa na milioni 2.5 walikimbia makazi yao katika mzozo wa Darfur katika miaka ya 2000.

Wakati wa kesi ya Kushayb, walionusurika walieleza jinsi vijiji vyao vilivyochomwa, wanaume na wavulana kuchinjwa na wanawake kulazimishwa kuwa watumwa wa ngono.

Jaji wa ICC anasema Kushayb alikuwa ametoa amri ya "kufuta na kufagia" makabila yasiyo ya Waarabu na kuwaambia wanajeshi "msimwache mtu yeyote nyuma. Msimlete mtu yeyote hai."

Wengi wa wapiganaji wa Janjaweed wamejiunga na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), kikundi cha wanamgambo ambacho kinapambana na jeshi la Sudan tangu Aprili 2023. Abd-Al-Rahman alikimbilia Jamhuri ya Afrika ya Kati Februari 2020 wakati serikali mpya ya Sudan iliposema itashirikiana na uchunguzi wa ICC.

Alisema alijisalimisha kwa sababu alikuwa "amekata tamaa" na alihofia viongozi wangemuua. Abd-Al-Rahman alikanusha mashtaka yote dhidi yake katika kesi hiyo, iliyofunguliwa Aprili 2022.

Hukumu hii  katika kesi ya kwanza na ya kipekee inayohusu uhalifu nchini Sudan tangu kesi hiyo kupelekwa mahakamani na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 2005.

Bado kuna kesi dhidi ya viongozi wengine kama rais wa zamani wa nchi hiyo Omar el Bashir.