Wajumbe la Bunge la Afrika Mashariki (EALA) linalokutana jijini Arusha, Tanzania limepitisha azimio la kupongeza baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuandaa kwa mafanikio mashindano ya CHAN 2024.
Kulingana na wajumbe hao, mafanikio hayo ni ishara ya umoja wa kikanda na weledi wa kimichezo ndani ya jumuiya hiyo yenye nchi wanachama nane.
Pongezi hizo zinakuja baada ya Tanzania, Kenya na Uganda, kuandaa michuano ya CHAN kwa pamoja.
Azimio hilo, lililowekwa mezani kwa kutumia ibara 49(2)(d), 59(1), 119(a) and (h) na sheria ya uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliletwa bungeni siku ya Oktoba 7, 2025 na Falhada Dekow Iman kutoka Kenya, huku likiungwa mkono na Clément Musangabatware wa Rwanda.
Kulingana na azimio hilo, nchini ya kifungu 119, nchi wanachama zimejitolea kushirikiana katika kukuza michezo na shughuli za kitamaduni, kama nyenzo ya kukuza utambulisho wa jumuiya hiyo.
Mwezi Agost 2025, Tanzania, Kenya na Uganda, ziliandaa kwa pamoja michuano ya CHAN 2024, ambayo ni maalumu kwa wachezaji wanaoshiriki ligi za ndani.
Wiki kadhaa baadaye, Rwanda iliandaa michuano ya kimataifa ya mbio za baiskeli, zilizofanyika kutoka Septemba 21 hadi 28, 2025.
"Nchi zetu zimeonesha, sio tu uwezo wake wa kuandaa michuano yenye hadhi ya kimataifa, bali utajiri wa kitamaduni, uzuri asilia na ukarimu wa watu wa Afrika Mashariki,” alisema Iman.