AFRIKA
2 dk kusoma
Polisi wa Tanzania kuchunguza madai ya kutekwa kwa mkosoaji wa serikali
Katika taarifa ya Septemba 29, serikali ilikataa madai ya Human Rights Watch kwamba inawakandamiza wakosoaji wake kabla ya uchaguzi na kutaja utekaji nyara "chanzo kikuu cha wasiwasi kwa serikali".
Polisi wa Tanzania kuchunguza madai ya kutekwa kwa mkosoaji wa serikali
serikali ilikataa madai ya Human Rights Watch kwamba inawakandamiza wakosoaji wake kabla ya uchaguzi / Reuters
tokea masaa 18

Jeshi la polisi nchini Tanzania limesema linachunguza ripoti kwamba balozi wa zamani aliyegeuka kuwa mkosoaji wa serikali alitekwa nyara baada ya familia yake kusema alichukuliwa kwa nguvu kutoka nyumbani kwake.

Wakosoaji kadhaa wa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anagombea tena kiti cha urais Oktoba 29, wametoweka tangu mwaka jana, huku vyama vya upinzani vikidai kampeni ya utekaji nyara.

Humphrey Polepole, ambaye alijiuzulu kama balozi wa Cuba mwezi Julai na mara kwa mara na kwa ukali amekua akikosoa chama tawala cha Tanzania , alitoweka nyumbani kwake katika mji mkuu wa kibiashara wa Dar es Salaam mapema Jumatatu, kwa mujibu wa kaka yake, Godfrey Polepole.

“Mlango mkuu wa kuingilia ndani ya nyumba hiyo ulivunjwa na mlango wa chumba cha kulala ulivunjwa pia,” alisema. "Kulikuwa na damu nyingi kutoka sebuleni hadi chumbani na madoa ya damu yaliendelea hata nje kuelekea eneo la lango."

Katika taarifa ya Septemba 29, serikali ilikataa madai ya Human Rights Watch kwamba inawakandamiza wakosoaji wake kabla ya uchaguzi na kutaja utekaji nyara "chanzo kikuu cha wasiwasi kwa serikali".

David Misime, msemaji wa polisi, alisema jeshi hilo linachunguza taarifa za kutekwa kwa Polepole.

“Jeshi la Polisi limeona taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na ndugu zake kuwa ametekwa, tayari tumeanza kuzifanyia kazi ili kubaini ukweli,” alisema katika taarifa yake juzi Jumatatu.

Baada ya kujiuzulu wadhifa wake, Polepole alizua msururu wa matukio mbalimbali wakati wa mkutano na waandishi wa habari mtandaoni dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akikituhumu kukiuka kanuni za chama kwa kumchagua Hassan kuwa mgombea wake wa urais, kujihusisha na ufisadi na kuwateka wakosoaji wa serikali.

CHANZO:Reuters