Zaidi ya vituo 200 vya afya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC eneo lililokumbwa na vita vimekosa dawa kutokana na kuenea kwa uporaji na usumbufu wa usambazaji wakati wa mapigano mwaka huu.
Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) ilisema haya Jumatano baada ya uchunguzi uliofanywa mwezi Septemba 2025, katika vituo vya afya na zahanati 240 katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini.
Hiyo ni tathmini kubwa zaidi ambayo ICRC imewahi kufanya tangu waasi wa M23 kuzusha mapigano ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu.
Takriban vituo tisa kati ya 10 vilivyofanyiwa uchunguzi havikuwa na dawa kikamilifu.
Uhaba wa wafanyakazi uliathiri 40% ya vituo vilivyofanyiwa utafiti, 13% havikuwa na kazi kabisa na nyingi ziliripoti uhaba wa usambazaji wa mara kwa mara kuanzia Januari, wakati M23 ilipoteka Goma, jiji kubwa zaidi katika kanda.
Rwanda imekanusha kwa muda mrefu kuunga mkono M23 na inasema vikosi vyake vinajilinda. Lakini kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa lilisema katika ripoti ya mwezi Julai kwamba Kigali ilitekeleza amri na udhibiti wa waasi.
Mgogoro wa huduma ya afya umefikia hatua duni huku mizozo ya kivita ikiongezeka na ufadhili wa kibinadamu ukipungua, alisema Francois Moreillon, mkuu wa ujumbe wa ICRC katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
ICRC ilionya kwamba maisha ya wakazi yako hatarini kwani malaria, VVU, kifua kikuu na magonjwa mengine hayatibiwi.
Amani Habimana, mkazi wa mji wa Ruke katika eneo la Masisi katika jimbo la Kivu Kaskazini, alipigwa risasi ya paja alipokuwa katika mapigano kati ya wapiganaji wa M23 na wanamgambo wa eneo hilo.
Familia yake ilimpeleka katika hospitali kadhaa ambapo madaktari walisema hawakuwa na vifaa muhimu vya kutibu mifupa yake iliyovunjika.
Hatimaye alifika katika jiji la Beni karibu miezi miwili baada ya tukio hilo.
Samson Muhindo Kalumbi, ambaye anafanya kazi katika ICRC katika hospitali kuu ya Beni, alisema matukio kama hayo ni vya kawaida, na wagonjwa wengi ambao wanatatizika kupata huduma hatimaye hufika Beni wakiwa na majeraha yaliyoambukizwa.
“Tunapoteza viungo vingi kutokana na umbali na kuchelewa kupata huduma,” alisema.
ICRC siku ya Jumatano ilitoa wito kwa pande zote kuhakikisha wahudumu wa afya wanapita salama katika maeneo yaliyokumbwa na vita, jambo ambalo litasaidia kupunguza uhaba wa wafanyakazi. M23 na serikali ya Congo haikujibu mara moja maombi ya maoni kuhusu matokeo ya ICRC.