Sudan imetaka jamii ya kimataifa na mashirika ya kikanda ya haki za binadamu kushtumu “uhalifu” unaofanywa na wapiganaji wa RSF dhidi ya raia na kuchukuwa hatua za haraka kuzuia hayo.
“Serikali ya Sudan inashtumu vikali uhalifu na ukiukwaji unaoendelea ambao unafanywa na wapiganaji wa RSF dhidi ya raia wasio na hatia, wasio na silaha, na kuharibu taasisi za serikali kwa maksudi, ikiwa ni ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu na maadili ya kimataifa,” Baraza la Kijeshi lilisema katika taarifa siku ya Jumamosi.
Lilisema serikali ‘‘inatoa wito kwa jamii ya kimataifa na mashirika ya haki za binadamu ya kikanda kushtumu ukatili unaoendelea na kuchukua hatua za haraka kuzuia uhalifu wa wapiganaji hao na kuwawajibisha wahusika, ili kulinda raia na kusimamia haki za binadamu”.
Mapema siku ya Jumamosi, jeshi la Sudan lilitangaza kuwa limefanya mashambulizi makubwa dhidi ya RSF huko Al Fasher, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini, magharibi mwa Sudan, kutoka maeneo matano, katika moja ya mapigano makali kuwahi kutokea kwenye mji huo katuka miezi kadhaa.
Katika wiki za hivi karibuni, mapigano kati ya jeshi la Sudan na wapiganaji wa RSF yameongezeka kote katik majimbo ya Kordofan na Darfur.














