AFRIKA
2 dk kusoma
Burkina Faso yakataa pendekezo la kupokea waliotimuliwa kutoka Marekani
Burkina Faso imesema imekataa pendekezo kutoka kwa serikali ya Rais Trump la kuwapokea watu waliotimuliwa kutoka Marekani.
Burkina Faso yakataa pendekezo la kupokea waliotimuliwa kutoka Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Burkina Faso Karamoko Jean Marie Traore./ / AP
tokea masaa 18

Waziri wa Mambo ya Nje, Karamoko Jean-Marie Traoré, alisema Alhamisi kupitia televisheni ya taifa kuwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi iliulizwa kama iko tayari kuwapokea watu wasio raia wa Burkina Faso waliotimuliwa na Marekani, pamoja na raia wake walioko uhamishoni.

“Kwa kawaida, pendekezo hili, ambalo tuliliona kama lisilo na heshima wakati huo, linapingana kabisa na thamani ya utu ambayo ni sehemu ya msingi wa maono ya Kapteni Ibrahim Traoré,” alisema, akimuashiria kiongozi wa wa nchi hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa saa chache tu baada ya Ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Ouagadougou kusitisha huduma nyingi za viza kwa raia wa Burkina Faso, na kuelekeza waombaji kuwasilisha maombi yao katika ubalozi wa Marekani katika nchi jirani ya Togo. Ubalozi haukutoa sababu ya hatua hiyo.

Kwa kunukuu waraka wa kidiplomasia kutoka Marekani unaodai kuwa raia wa Burkina Faso hawakufuata sheria za matumizi ya viza, Karamoko Jean-Marie Traoré alieleza kuwa huenda hii ni “njia ya kuishinikiza” nchi hiyo na kuongeza kuwa, “Burkina Faso ni nchi ya heshima, si ya kutupia watu waliotimuliwa.”

Ubalozi wa Marekani nchini Burkina Faso na Idara ya Usalama wa Ndani ya Marekani hawakujibu mara moja maombi ya maoni juu ya suala hilo.

Tangu Julai, zaidi ya watu 40 waliotimuliwa wametumwa barani Afrika baada ya utawala wa Trump kufikia makubaliano ya siri na takriban mataifa matano ya Afrika kuwapokea wahamiaji chini ya mpango mpya wa kuwatimua wahamiaji kwenda nchi ya tatu. Makundi ya haki za binadamu na wengine wamepinga mpango huo.

Marekani imewatuma waliotimuliwa katika mataifa madogo ya Afrika kama vile Eswatini, Sudan Kusini, Rwanda, na Ghana. Pia ina makubaliano na Uganda, ingawa bado hakuna waliotimuliwa waliotangazwa kupelekwa huko.

Watu sita waliotimuliwa bado wanazuiliwa katika kituo kisichojulikana nchini Sudan Kusini, huku Rwanda haijatangaza walipo watu saba waliowapokea.

Kati ya watu 14 waliotimuliwa na kupelekwa Ghana mwezi uliopita, 11 waliishtaki serikali kwa kuwaweka katika mazingira mabaya katika kambi ya kijeshi pembezoni mwa mji mkuu, Accra.

CHANZO:AP