ULIMWENGU
1 dk kusoma
Trump: Itakuwa ni ‘dhihaka’ kwa Marekani kama nisiposhinda Tuzo ya Amani ya Nobel
Siku ya Jumanne, Trump alisisitiza kuwa ameshiriki katika utatuzi wa migogoro saba, tangu kuingia kwake madarakani mwezi Januari mwaka 2025.
Trump: Itakuwa ni ‘dhihaka’ kwa Marekani kama nisiposhinda Tuzo ya Amani ya Nobel
Rais Donald Trump wa Marekani./Picha:Wengine
30 Septemba 2025

Rais wa Marekani Donald Trump amejinasibu kuwa anaweza kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel, akiongeza kuwa itakuwa ni dhihaka kwa taifa lake iwapo ataikosa tuzo hiyo.

Akizungumza siku ya Jumanne, Trump amedai kuwa anastahili tuzo hiyo kutokana na nafasi yake katika usuluhishi wa migogoro na vita ulimwenguni.

Katika hotuba yake aliyoitoa siku ya Jumanne, Trump alisema kuwa alihusika na kusuluhisha migogoro saba ya kisiasa, tangu alipoingia madarakani mwezi Januari mwaka huu.

“Itakuwa dhihaka kubwa sana kwa nchi yetu, wacha nikuambie tu. Siihitaji tuzo hiyo binafsi, nataka nchi yangu ishinde,” alisema.

Trump, ambaye anatokea chama cha Republican, ameonekana kukerwa na uhalisia kwamba Barack Obama, kutoka Democrat aliwahi kushinda tuzo hiyo mwaka 2009.

Siku ya Jumanne, Trump alisisitiza kuwa ameshiriki katika utatuzi wa migogoro saba, tangu kuingia kwake madarakani mwezi Januari mwaka 2025.

Hivi karibuni, utawala wa Trump, ulianisha migogoro saba ambayo kiongozi huyo alihusika kuitatua ambayo ni Cambodia dhidi ya Thailand; Kosovo dhidi ya Serbia, DRC dhidi ya Rwanda, Pakistan dhidi ya India, Israel dhidi ya Iran, Misri dhidi ya Ethiopia na Armenia dhidi ya Azerbaijan.

CHANZO:AFP