Kila alfajiri jijini Mogadishu, miale ya kwanza ya jua inapokatiza uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Aden Abdulle, Nahodha Yasmin hutembea kwenye uwanja huo kwa kujiamini, akiwa amevalia sare rasmi, huku akiwa amebeba kifaa cha mawasiliano.
Anapoketi kwenye kiti cha kushoto cha rubani mkuu ndani ya ndege, huwasilisha mfumo wa uendeshaji wa ndege, hukagua vifaa vya kuonesha hali ya ndege, huangalia viwango vya injini, na kupitia orodha ya maandalizi kabla ya safari.
Wakati huo, wahudumu wengine wakiendelea kupanga mizigo na kufunga milango ya ndege. Ndani yake, Yasmin huhakikisha kila mfumo uko katika hali bora kabla ya kutoa idhini ya kuanza kwa safari.
Ni utaratibu wa nidhamu na umakini unaoashiria mwanzo wa siku nyingine ya kuwapeleka abiria hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, jijini Nairobi.
Kwa miaka saba sasa, mwendo huu wa kuamka mapema, kuruka katika mwinuko wa wastani, na kutua kwa ustadi, umekuwa sehemu ya maisha yake ya kila siku.
Katika urefu wa futi 35,000, Yasmin haendeshi tu ndege, anabeba pia uzito wa historia. Kila anapoinua ndege kutoka ardhi ya Somalia, huvunja vizuizi vilivyojengwa kwa wanawake.
Vizazi vya wasichana wa Kisomali vilikua vikimsikia tu Asli Hassan Abade, shujaa na rubani wa kwanza wa kike aliyeruka anga kati ya miaka ya 1970 na 1990.
Sasa, akiwa na mikono thabiti kwenye usukani na macho yaliyokazia upeo wa macho, Nahodha Yasmin anaandika ukurasa mpya, unaogeuza matumaini kuwa uhalisia, na kuthibitisha kuwa anga ya Somalia haijatengwa kwa wanaume pekee.
‘Rubani Bora wa Mwaka’Mnamo Mei 2022, katika hafla iliyofanyika kwenye Uwanja wa Ndege wa Aden Adde jijini Mogadishu, Yasmin alipandishwa rasmi kuwa rubani mpya wa ndege; kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo baada ya zaidi ya miongo mitatu.
Tangu wakati huo, Yasmin amesharusha ndege kwa saa nyingi hewani, akivuka anga ya Somalia kwa ustadi na utulivu. Yasmin hufanya safari za kimataifa kati ya Kenya, Djibouti na Somalia, na pia safari za ndani ndani ya mipaka ya Somalia.
Baada ya miongo kadhaa bila mwanamke katika chumba cha rubani, mafanikio ya Yasmin yanawakilisha mapinduzi ya kijamii kwa kizazi kipya.
Alizaliwa katika Kaunti ya Wajir nchini Kenya, jamii yenye mizizi imara ya Kisomali, na safari yake kutoka Wajir hadi juu ya anga ya Mogadishu ni simulizi ya ajabu ya kujitolea na azma.
Akiwa na umri wa miaka 27, si rubani tu, bali ni mhamasishaji anayebeba historia kila anapoketi kwenye kiti cha nahodha.
“Hili ni ushuhuda kwa wanawake wa Kisomali kila mahali,” alisema baada ya kutunukiwa tuzo ya Rubani wa Mwaka wa Somalia 2025 jijini Mogadishu.“
Inathibitisha kuwa wanawake wana nafasi kwenye kiti cha rubani. Kila mara ninaposhika usukani wa ndege, sibebi tu abiria, bali ndoto za wasichana wadogo wenye uthubutu.
”Kuvunja vizingiti
Safari yake haikuwa nyepesi. Kama wanawake wengi wanaojaribu kufaulu katika taaluma ya usafiri wa anga, Yasmin alikumbana na upinzani. Baadhi walitilia shaka uwezo wa wanawake kuendesha ndege kwa usalama.
Hata hivyo, kupitia bidii, mafunzo, na nia thabiti, aliweza kuvunja mashaka hayo yote. Chini ya uongozi na uelekezi wa mtaalamu wa usafiri wa anga, Osman Abass Amin, kupitia Maandeeq Air, Yasmin alihitimu masomo yake na kupata ujasiri wa kuwa rubani mkuu.
“Ndoto yake tangu utotoni ilikuwa kuwa rubani. Alikuwa mchapa kazi na mwenye malengo. Kama familia, tunajivunia juhudi na mapenzi yake kwa taaluma hii.
Tunamuombea kila wakati,” anasema dada yake mkubwa, Hamdi Abdi, akizungumza na TRT Afrika.
Kwa mara nyingine tena, Yasmin ametunukiwa tuzo ya Rubani Bora wa Mwaka.
Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Shueib Ali Warsame, alimweleza Yasmin kama “kielelezo cha ubora katika sekta ya anga ya Somalia,” na kumsifu kwa kuleta imani kwa wateja na wadau wa sekta hiyo.
“Hongera tena, Kapteni,” shirika lilitangaza kwa fahari.
Kielelezo kwa Jamii
Kwa wazazi wake, Yasmin ni baraka ya kweli.
“Yasmin amekuwa zawadi kwa familia yetu tangu alipozaliwa. Alikuwa akiongoza katika masomo shuleni na alifanya vizuri kitaaluma. Amekuwa na mchango mkubwa kwa familia na marafiki. Ni mtu wa amani, mnyenyekevu, asiyekuwa na hasira. Kama wazazi wake, tumekuwa tukimwombea yeye na familia nzima,” anasema mama yake, Habiba Bulle, akizungumza na TRT Afrika.
“Kuona akitimiza ndoto yake ya kuwa rubani ni mojawapo ya furaha yetu kuu. Alikuwa na ndoto ya kuruka angani, na ndugu zake walikuwa pamoja nasi katika kumuunga mkono. Tunaamini katika umuhimu wa kujitolea kwa ndoto za watoto wetu. Ili kufanikisha ndoto yake, tuliuza mifugo yetu na hata shamba la familia. Hilo lilikuwa bei ndogo kulinganisha na furaha ya kumuona akiruka angani,” anasema Habiba.
Sekta ya anga, ambayo hapo awali iliharibiwa na migogoro, sasa imeanza kushamiri tena.
Maboresho ya sera, teknolojia, na kurejea kwa wataalamu waliopotea vimeleta mapinduzi katika usafiri wa anga.
Ndani ya mabadiliko hayo, simulizi ya Yasmin inang’aa zaidi, si tu kwamba Somalia imejenga upya anga yake, bali pia imefungua milango kwa wanawake kuiongoza.
“Leo hii, anaendelea kuwahamasisha wadogo zake na wasichana wengine kuifuata njia yao wenyewe na kufuata ndoto zao. Tunatumai simulizi yetu itawahamasisha wazazi wote kuunga mkono ndoto za watoto wao, bila kujali gharama,” anasema mama yake.
Tuzo alizopokea; Rubani Bora wa Mwaka 2024 katika SomTex Industry Awards, na Rubani Bora wa Mwaka 2025 katika Somali Travel & Tourism Expo, ni uthibitisho kuwa mafanikio yake yanazidi kukua. Kwa wasichana wa Kisomali wanaomuona akipanda ndege, Yasmin anatoa ujumbe huu: “Kwa kila msichana wa Kisomali anayeota kuwa rubani, inawezekana.”