Uzalishaji wa mkonge duniani unakadiriwa kufikia takriban tani 300,000, ambazo zina thamani ya dola milioni 75.
Mzalishaji mkuu wa mkonge duniani ni Brazil lakini hapa barani Afrika Tanzania inaongozwa ikifuatiwa na Kenya.Inasemekana mkonge, asili yake ni maeneo makame ya kule Marekani ya kaskazini na kati.
Mmea huo, kwa mara ya kwanza ulianzishwa katika eneo la Afrika Mashariki mwaka 1893, wakati huo ikiwa ni Tanganyika.
Mwanzilishi wake akiwa ni Dkt. Hindorf, mwanasayansi wa Kijerumani.
Mimea ya kwanza ya mkonge katika Afrika Mashariki ilipandwa Kikogwe upande wa kusini wa Mto Pangani katika mkoa wa Tanga nchini Tanzania kwenye ukingo wa eneo ambalo sasa ni eneo la Mwera.
Uzalishaji wa mkonge ulikuwa na ufanisi mkubwa Afrika Mashariki na kufikia mwishoni mwa miaka ya 1960 ulisambaa katika nchi jirani ya Kenya.
Takwimu rasmi kati ya Januari na Juni 2025 zinaonesha Tanzania iliuza takriban tani 18,990 za mkonge ziliuzwa nje ya nchi na Kenya iliuza takribani tani 11,500 za mkonge huku Madagascar ikiuza wastani wa tani 2,600.
Soko kubwa la mkonge linasukumwa na sekta ya ujenzi ambapo bidhaa zake zinatumika kuweka plasta na dari yaani gypsum.
Wanunuzi wakubwa wa mkonge ni nchi kama vile China, Nigeria, Ghana, Morocco, India, Saudi Arabia na Misri.Kienyeji, mkonge hutumika kutengenezea kamba, mifuko, mazulia, vikapu na samani, wakati kimataifa hutumika katika utengenezaji wa karatasi, mbao za dari, vifaa vya magari, nguo na hata fedha za karatasi.
Upandaji wa mkonge unahitaji vipindi virefu vya jua ili kuwa na singa nyingi na nzito. Hivyo hautakiwi kupandwa kwenye kivuli.
Uvunaji unaweza kufanywa baada ya miaka mitatu kwa majani yaliyokomaa huku majani yanayotakiwa kuvunwa ni lazima yasipungue urefu wa sentimita 60.
Majani huvunwa kutumia kisu kikali na kukatwa kwenye eneo ambalo jani linaungana na shina.
Ukishavunwa unatakiwa kusindikwa ndani ya saa 48 baada ya kuvunwa ili kupata nyuzi bora.
Mkonge uliokomaa huvunwa mara tatu kwa mwaka na mkulima anaweza kupata hadi dola 1,850 kwa mwaka kutoka kwa ekari moja.
Mmea mmoja unaweza kuvunwa kwa miaka 10.
Mahitaji ya nyuzinyuzi za mkonge hata hivyo yanatishiwa na mabadiliko ya tabia nchi na ushindani kutoka kwa nyuzi za sintetiki huku pia kukiwa na mabadiliko ya upendeleo wa soko.