Utajiri wa Afrika: Mafuta ya Angola
Utajiri wa Afrika: Mafuta ya Angola
Sekta ya nishati inasalia kuwa muhimu nchini Angola ikichukua karibu asilimia 75 ya pato la serikali
3 Oktoba 2025

Angola ina utajiri mwingi wa mafuta ambayo hayajatumika.Ni nchi ya pili barani Afrika kwa uzalishaji mkubwa wa mafuta baada ya Nigeria.

Nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika mbali na mafuta, pia ina rasilimali nyingi ya gesi ambayo haijatumika. 

Ina wastani wa mapipa ya akiba ya mafuta bilioni 9 ambayo hayajasafishwa na futi za ujazo trilioni 11 za hifadhi ya gesi asilia iliyothibitishwa.

Hivi sasa inazalisha zaidi ya mapipa milioni 1 kwa siku ambayo kiwango kidogo cha uzalishaji wa karibu mapipa milioni 2 kwa siku mwaka 2008.

Sekta ya nishati inasalia kuwa muhimu, ikichukua karibu asilimia 75 ya pato la serikali.

Mnamo Disemba 2023, Angola ilijiondoa rasmi kutoka Shirika la Nchi Zinazouza Petroli, OPEC baada ya kutofautiana kuhusu viwango vya uzalishaji.

Lengo lilikuwa ni kutaka kurejesha uhuru zaidi juu ya mkakati wake wa uzalishaji wa mafuta, ikilenga kuongeza pato katika soko la kimataifa la ushindani la mafuta.

Mnamo Disemba 2024, Angola ilianza kuongeza pato la gesi kutoka kwa Mradi wa Kuunganisha Gesi ya Sanha Lean, awali ikizalisha takriban futi za ujazo milioni 80 kwa siku.

Hata hivyo, pamoja na utajiri huu wote nchi inategemea matumizi ya petroli kutoka nje ya nchi zaidi ya dola bilioni 2 kwa uagizaji wa petroli kila mwaka.

Wataalamu wanasema sehemu ya tatizo ni utegemezi mkubwa wa mafuta wa Angola, ambayo ni zaidi ya asilimia 60 ya mapato ya serikali na asilimia 95 ya mauzo ya nje.Hata hivyo, nchi inazalisha takriban asilimia 30 tu ya mahitaji yake ya ndani ya matumizi ya mafuta.

Nchi hiyo iliegemeza bajeti yake ya 2025 kwa bei ya mafuta ya $70 kwa pipa, lakini matarajio ya bei ya kimataifa ilishuka chini ya $60 mwezi Aprili baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutangaza ongezeko kubwa la ushuru.

Wataalamu wanasema changamoto nyingine ni pamoja na urasimu unaoendelea, kukosekana kwa uwazi katika manunuzi na leseni, kutofuata kanuni za udhibiti na upatikanaji mdogo wa fedha za kigeni.

Ushuru tata na gharama kubwa ya uendeshaji pia huathiri mapato kutoka kwa sekta ya mafuta.Nchi inajitahidi kushughulikia hili kupitia kuimarisha sera za uzalishaji na vilevile Angola inatanguliza maendeleo ya usafishaji.