Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza James Cleverly na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Vincent Biruta walitia saini makubaliano hayo mjini Kigali nchini Rwanda. Picha: James Cleverly

Uingereza na Rwanda zimetia saini mkataba mpya Jumanne katika jitihada za kufufua pendekezo linaloonekana kuwa na utata la Uingereza la kuwahamisha wahamiaji katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki ambalo lilipingwa na mahakama ya Uingereza.

Makubaliano hayo, ambayo, kulingana na Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak ni muhimu kutimiza ahadi yake ya kukata uhamiaji usio wa kawaida kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa mwaka ujao, ulisainiwa mjini Kigali.

Mataifa hayo mawili yanawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza James Cleverly na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Vincent Biruta ambao walitia saini makubaliano hayo kwa niaba ya nchi zao.

Waziri James Cleverly wa Uingereza, alisafiri hadi mji mkuu wa Rwanda kuokoa mpango huo wa London wa kuwatuma wahamiaji hadi Rwanda baada ya mahakama kuu ya Uingerza kutaja mpango huo kuwa kinyume cha sheria.

"Tunaamini wazi kwamba Rwanda ni nchi salama, na tunafanya kazi kwa kasi ili kusonga mbele na ushirikiano huu ili kusimamisha boti na kuokoa maisha," Cleverly alisema.

Uingereza imejitetea kuwa, chini ya mkataba huo mpya, Rwanda itadhibitiwa na sheria ya kimataifa ya kutorudisha watu katika nchi ambayo maisha yao au uhuru wao utakuwa hatarini.

AFP