Chama kikuu cha upinzani nchini Sudan Kusini, Sudan People’s Liberation Movement in Opposition (SPLM-IO) kimesema kuwa kusimamishwa kazi kwa kiongozi wake Dkt. Riek Machar kumemaliza uhalali wa serikali ya amani ya 2018.
Makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar, alisimamishwa kazi kwa muda baada ya kushtakiwa kwa makosa ya mauaji, uhaini na uhalifu dhidi ya binadamu kwa madai ya kuhusika katika mashambulizi yaliyofanywa na kundi la ‘White Army’ dhidi ya vikosi vya serikali mwezi Machi 2025.
Chama hicho kimekataa mashtaka dhidi ya Machar.
“Tunatoa wito kwa wanaounga mkono, wafuasi wake wa kisiasa na kijeshi kujitokeza kwa huduma ya kitaifa ya jeshi, ili kulinda wananchi wa nchi hiyo na kutumia mbinu zote kuikomboa nchi,” SPLM/IO imesema katika taarifa.
Serikali hii ya mpito iliundwa kwa makubaliano kati ya serikali ya Sudan Kusini chini ya Rais Salva Kiir, upande wa upinzani SPLM-IO na vyama vyengine kwa ajili ya kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyotokea kati ya 2013 na 2018.
Utekelezaji wa makubaliano hayo ulianza 2020 na kuundwa kwa serikali ya pamoja ambapo Riek Machar aliteuliwa kama Makamu wa Rais.
Baada ya Riek Machar kushtakiwa kwa uhaini, Rais Kiir alitoa amri ya kumfuta kazi.
“Kusimamishwa kazi kwa Makamu wa Rais wa kwanza wa Sudan kusini, ni ukiukwaji mkubwa wa makubalioni ya amani ya 2018, na makubaliano ya masuala ya kisiasa na usalama,” SPLM/IO imesema katika taarifa.
“SerikalI iliyoundwa ya amani imeharibika pamoJa na mifumo yake,” chama hicho kimeongezea.
Chama cha Machar Kinaonya pia kuwa uongozi wa sasa wa Sudan Kusini hauna msingi wa makubaliano ya amani ila kwa uongozi wa nguvu.
Serikali ya Rais Salva Kiir haijatoa majibu kuhusu maoni ya chama cha Machar kuitisha suluhisho ya kivita.