Kenya na kitendawili cha ibada za kishetani
AFRIKA
5 dk kusoma
Kenya na kitendawili cha ibada za kishetaniMkasa wa Shakahola sio tukio la pekee. Kesi za awali, kama vile ugunduzi wa 1999 wa dhehebu katika kijiji cha Opapo, ulihusisha mazishi ya siri na tambiko za ibada. Licha ya maonyo haya, hatua ya serikali imekua dhaifu.
Ibada za miungu na tambiko za kishirikina Kenya / Getty Images
16 Septemba 2025

Na Dayo Yussuf

Waswahili wa pwani ya Afrika Mashariki wana msemo maarufu usemao: Kashangae feri, shilingi inazama, meli inaelea.’ Msemo huu unasadifu tukio la makaburi yaliyogundulika katika misitu ya Shakahola pwani ya Kenya.

Jambo hili si geni nchini Kenya, japo kwa wengine, linaweza kuwa la kushtua.

Kumekuwepo na madai ya uwepo wa nyumba za ibada maarufu kama ‘Nyumba za Shetani’, tangu kugundulika kwa makaburi ya Shakahola ambako zaidi ya miili 400 ilifukuliwa.

Inasemekana kuwa, ni ndani ya ‘nyumba hizo za ibada’ ambamo, viongozi wa ‘makundi’ hayo huwashawishi waumini wao kufanya kila aina ya tambiko ili kupata wokovu. Mara nyingine, wafuasi wa makundi haya huambiwa wasilimishe mali zao kwa viongozi wa makundi hayo au kujinyima vinywaji na vyakula.

Hali hii, hupelekea baadhi ya wafuasi kudhoofika kiafya, na wengine ‘kupoteza maisha, kwa jina la imani’.

Utumwa wa kiakili

Kila kukicha, watu mbalimbali hujitokeza na kudai kuwa wamajeliwa nguvu za ajabu, na uchao watu wanajitokeza kudai kuwa ‘mungu’ na ajabu ni kuwa idadi ya wafuasi wao, inakuwa siku hadi siku.

“Umaskini ni kitu kinachofungamana na akili ya mtu,’’ anasema Dkt Kennedy Ongaro Mkurugenzi wa masomo ya sera na maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Daystar jijini Nairobi.

‘‘Kwa hiyo unapomuambia mtu una suluhisho la matatizo yake na unaweza kumtoa katika umaskini, atafuata chochote kile utakachomuambia. Ndio maana unaona waumini wa Shakahola, waliambiwa wapeleke kila kitu wanachomiliki kwa mchungaji wao na wakaleta,’’ Dkt Ongaro anaambia TRT Afrika.

Tukio hili la kusikitisha linaangazia wasiwasi ulioibuliwa miongo kadhaa wakati wa utawala wa Rais Daniel Arap Moi.

Mnamo Oktoba 1994, Rais Moi aliunda tume maalumu ya kuchunguza madai ya ibada za shetani nchini Kenya.

Ikiongozwa na Askofu Mkuu wa Nyeri wa wakati huo, Nicodemus Kirima, matokeo ya tume yalikuwa ya kushangaza na ya kustaajabisha.

Kupumbazwa kiroho

Wengi waliohojiwa na tume hiyo walikuwa wanachama wa zamani ambao walielezea ibada za kufundwa, mbinu za kudhibiti akili na tambiko za mara kwa mara.

Tume ilibaini muunganiko na uthabiti katika maelezo katika simulizi tofauti za mashahidi na ikapata alama za makovu na chanjo na vifaa vinavyounga mkono baadhi ya shuhuda.

“Kulikuwa na kiwango cha juu cha uthabiti katika shuhuda nyingi na kwa hivyo kuhitimisha ibada ya kuabudu shetani ilikuwepo nchini Kenya, na baadhi ya matambiko yaliyorekodiwa yalikuwa ya hatari na uhalifu,’’ ilielezea sehemu ya ripoti ya tume hiyo.

Tume ilithibitisha uwepo mkubwa wa ibada ya shetani, haswa miongoni mwa vijana na vikundi vya watu wasiojiweza kiuchumi.

‘‘Imani ya kiroho siku zote ndio kina. Inatokana na ukosefu wa uelewa wa masuala ya kiroho na ki Mungu, kwa hiyo kwa wale wanaotafuta utakaso au wokovu katika dini wanaamini na kufuata chochote kinachowaahidi uzima wa milele. Au uponyaji, bila kuuliza masuali. wanaamini kitambaa cheupe walichopewa na mchingaji, mafuta au maji ya uponyaji au tambiko zingine. Wakati mwingine hizo tambiko zinawadhuru au kusababisha kifo,’’ anaongeza Dkt. Ongaro.

Mila za wazee

Ushuhuda ulifunua matumizi ya udhibiti wa akili, mila ya kufundwa na alama za uchawi, kama vile michoro ya pentagram na nambari 666.

Dalili zote zinaonyesha kuwa hiki ni kitu kilichokita mizizi miaka mingi sana nyuma.

‘‘Watu hawataki kuachana na mila za wazee wao. wengine wanaogopa kulaaniwa kwa hiyo unakuta imani hizi zinapitishwa kwa vizazi,’’ anasema Dkt. Ongaro.

Tukimulika mbele zaidi hadi 2023, msitu wa Shakahola katika Kaunti ya Kilifi ukawa eneo la mikasa ya kuogofya zaidi nchini Kenya inayohusiana na ibada. Wakiongozwa na Paul Mackenzie, shirika la Good News International Ministries liliwashawishi wafuasi katika kufunga hadi kufa, wakiamini kuwa ingewaongoza kwenye wokovu.

Mazoea ya kidini bila udhibiti

Zaidi ya watu 400 walifariki, huku miili mingi ikipatikana kwenye makaburi yenye kina kifupi. Baadhi waliokolewa wakiwa hai lakini walinusurika kwa unyoya. Mackenzie na washirika kadhaa walikabiliwa na mashtaka, yakiwemo ugaidi na mauaji.

Tukio hili lilionyesha kwa uwazi hatari za mazoea ya kidini yasiyodhibitiwa na kushindwa kwa serikali kutekeleza sheria zilizopo.

‘‘Hatuna sera muafaka na sheria za kudhibiti shughuli za ibada ya shetani au udanganyifu wa kidini. Katika nchi nyingine, ni uhalifu kisheria kutumia dini kuhadaa watu. Ukikamatwa ukishirikisha watu katika matambiko haya ya kishetani unakamatwa na kufungwa. Wengi wamekamatwa, wameshitakiwa, lakini tunawaona wameachiliwa ghafla na hakuna adhabu,’’ Dkt. Ongaro anaambia TRT Afrika.

Mkasa wa Shakahola sio tukio la pekee. Kesi za awali, kama vile ugunduzi wa 1999 wa dhehebu katika kijiji cha Opapo, ulihusisha mazishi ya siri na tambiko za ibada. Licha ya maonyo haya, hatua ya serikali imekua dhaifu.

Rejelea mapendekezo ya Tume ya 1994

Kwa bahati mbaya, mapendekezo ya Tume ya Kirima ya 1994 yalipuuzwa na tume kuvunjwa ghafla. Lakini Ili kuzuia majanga zaidi, wataalamu wameshauri umuhimu wa Kenya kurejelea mapendekezo ya tume hiyo.

Tume ilipendekeza kuundwa kikosi kazi maalum ndani ya polisi ili kufuatilia na kuchunguza shughuli za ibada.

Pia ilitaka kusasishwa sheria ili kushughulikia ibada za shetani za kisasa na kuhakikisha kuwa zinatekelezwa, na Kuelimisha umma, haswa vikundi vilivyo hatarini, kuhusu ishara na hatari za madhehebu za kuibuka.

‘‘Kuibuka tena kwa imani za kidini nchini Kenya, na kufikia kilele cha mauaji ya Shakahola, kunasisitiza haja ya haraka ya hatua za kina za kukabiliana na tishio hili,’’ anasema Dkt. Ongaro. ‘‘Kwa kujifunza kutokana na ripoti za zamani na kuchukua hatua madhubuti, Kenya inaweza kuwalinda raia wake kutokana na athari mbaya za uvutano wa madhehebu.’’ anaongeza.

CHANZO:TRT Afrika Swahili