AFRIKA
1 dk kusoma
Mahakama ya Kenya yatoa hati ya kukamatwa kwa raia wa Uingereza kufuatia mauaji ya Agnes Wanjiru
Kulingana na Alexander Muteti, ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Nairobi, kulikuwa na sababu za kutoa hati ya kukamatwa kwa mshukiwa huyo ambaye ni mkazi wa Uingereza.
Mahakama ya Kenya yatoa hati ya kukamatwa kwa raia wa Uingereza kufuatia mauaji ya Agnes Wanjiru
Ndugu wa Agnes Wanjiru./Picha:Wengine
16 Septemba 2025

Mahakama ya jijini Nairobi, siku ya Jumanne iliwasilisha hati ya kukamatwa kwa raia wa Uingereza anayehusishwa na mauaji ya binti wa Kikenya, ambaye mwili wake uliopolewa kutoka shimo la maji machafu, zaidi ya miaka kumi iliyopita.

Agnes Wanjiru, alifariki dunia mwaka 2012, baada ya kuripotiwa kutoka kwenye starehe akiwa pamoja na askari wa Uingereza katika mji wa Nanyuki ambako wanajeshi hao wameweka ngome yao.

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ilisema kuwa ushahidi uliokusanywa, unamhusisha askari huyo katika mauaji hayo.

Kulingana na Alexander Muteti, ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Nairobi, kulikuwa na sababu za kutoa hati ya kukamatwa kwa mshukiwa huyo ambaye ni mkazi wa Uingereza.

Kufuatia hukumu hiyo, kupitia ukurasa wake wa X, ofisi ya DPP ilisema mchakato wa kumleta mshukiwa huyo nchini Kenya utaanza kushughulikiwa.

Kwa upande wake, dada wa Wanjiru, Rose Wanyua Wanjiku, alipongeza maamuzi hayo akisema ni vyema haki ionekane bayana ikitendeka.

"Tuna furaha kubwa kama familia, kwani imetuchukua miaka mingi ya kusubiri, na kwa sasa tunaona hatua kubwa ikiwa imepigwa," alisema.

CHANZO:AFP