AFRIKA
2 dk kusoma
Vurugu Niger: Wenyeji waliuawa wakati wa sherehe ya ubatizo
Mashambulizi haya yametokea katika mkoa wa Tillaberi, karibu na Burkina Faso na Mali, ambapo vikundi vya watuhumiwa vinavyohusishwa na Al-Qaeda na Daesh viko hai.
Vurugu Niger: Wenyeji waliuawa wakati wa sherehe ya ubatizo
Askari wa Niger wamekuwa wakipambana na makundi ya kigaidi katika eneo lenye vurugu la Tillaberi. / Reuters
tokea masaa 8

Watu wenye silaha waliokuwa wakitumia pikipiki waliwaua watu 22 katika kijiji cha magharibi mwa Niger, wengi wao wakiwa wanahudhuria sherehe ya ubatizo, vyombo vya habari vya ndani na vyanzo vyengine viliripoti Jumanne.

Mauaji hayo yalitokea Jumatatu katika eneo la Tillaberi, karibu na mipaka ya Burkina Faso na Mali, ambako makundi ya kigaidi yanayohusishwa na Al-Qaeda na Daesh yanafanya shughuli zao.

Mkazi mmoja wa eneo hilo aliiambia AFP kwamba watu 15 waliuawa kwanza katika sherehe ya ubatizo katika kijiji cha Takoubatt.

“Washambuliaji kisha walielekea pembezoni mwa kijiji cha Takoubatt ambako waliwaua watu wengine saba,” alisema mkazi huyo, ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa sababu za kiusalama.

Chombo cha habari cha ndani, Elmaestro TV, kiliripoti “idadi ya kutisha ya vifo vya watu 22 wasio na hatia waliouawa bila sababu yoyote.”

“Kwa mara nyingine tena, eneo la Tillaberi limekumbwa na ukatili, likiwatumbukiza familia zisizo na hatia katika majonzi na kukata tamaa,” alisema mwanaharakati wa haki za binadamu wa Niger, Maikoul Zodi, kupitia mitandao ya kijamii.

Wanajeshi waliouawa

Serikali ya Niger imekuwa ikijitahidi kudhibiti makundi ya kigaidi katika Tillaberi, licha ya kuwepo kwa idadi kubwa ya wanajeshi katika eneo hilo. Takriban wanajeshi 20 waliuawa katika eneo hilo wiki iliyopita.

Shirika la Human Rights Watch limeitaka serikali ya Niger “kufanya zaidi kuwalinda” raia dhidi ya mashambulizi ya kikatili.

Kundi hilo la ufuatiliaji wa haki linakadiria kuwa makundi ya kigaidi yamewaua kwa “kuwafyatulia risasi moja kwa moja” zaidi ya wakazi 127 na waumini wa Kiislamu katika Tillaberi katika mashambulizi matano tangu Machi.

Wakati huo huo, shirika la ACLED, ambalo linafuatilia waathiriwa wa migogoro duniani kote, linasema kuwa takriban watu 1,800 wameuawa katika mashambulizi nchini Niger tangu Oktoba 2024 — robo tatu ya vifo hivyo vikiwa Tillaberi.

Niger na majirani zake, Burkina Faso na Mali, wanakabiliana na changamoto zinazoendelea za ugaidi.