Na Hamisi Iddi Hamisi
Katika historia ya siasa kinyang’anyiro cha Uchaguzi nchini humo, unapotaja vyama vya upinzani huwezi kukamilisha orodha yako bila kutaja Chama cha Wananchi – Civic United Front (CUF).
CUF ikiwa imeshiriki katika Uchaguzi Mkuu mara 6, ni mara 5 tu ndio ilisimika mgombea wa Urais na kushindwa mara zote.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Chama hicho kimemteua Gombo Samandito Gombo kuwa mgombea wa Urais na Husna Mohamed Abdallah kuwa mgombea mwenza.
Gombo ni mzaliwa wa Kanda ya Ziwa yani jijini Mwanza, lilipo Ziwa Victoria lenye Samaki watamu aina ya sato.
Mbali na siasa, Gombo anajishughulisha na kazi zake za kilimo na ufugaji. Kitaaluma mwana Samandito ni mjuzi wa Uboreshaji wa Nyumba na Maendeleo ya Miji, elimu ambayo aliisomea katika chuo kikuu cha Erasmus University Rotterdam huko Uholanzi.
Agosti 13 mwaka huu, Gombo Samandito akiambatana na mgombea mwenza Husna Abdallah, alichukua fomu ya kuteuliwa kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Msisitizo wa Gombo umejikita katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za kijamii kwa haki bila ubaguzi wowote bila kuangalia uwezo wa kifedha.
Ikumbukwe kuwa Gombo aliyekuwa mjumbe wa halmashauri kuu chama cha UMD, mwezi Machi tu mwaka 2025 alichukua na kurudisha fomu ya kuomba chama hicho kimteue kugombea nafasi ya urais.
Lakini baadaye kutokana na sintofahamu iliyotokea ilimfanya atimkie chama cha wananchi CUF na mwezi Agosti kikamteua na kumpa ridhaa ya kuwania nafasi hiyo.