AFRIKA
2 dk kusoma
Chama cha PFF cha Uganda chajiondoa katika kinyang’anyiro cha kugombea Urais 2026
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda wa chama cha PFF, Kizza Besigye, tangu awekwe kizuizini hivi sasa zimetimia siku 300. Besigye anashikiliwa kwa madai ya kumiliki silaha kinyume cha sheria pamoja na uhaini.
Chama cha PFF cha Uganda chajiondoa katika kinyang’anyiro cha kugombea Urais 2026
Kizza Besigye na mwenzake Obeid Lutale wametiwa mbaroni walipokuwa nchini Kenya Novemba 16, 2024. / / Reuters
16 Septemba 2025

Katika hatua kubwa ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2026, chama cha upinzani cha People’s Front for Freedom (PFF), kinachohusishwa na mwanasiasa mkongwe wa upinzani Kizza Besigye, kimetangaza rasmi kuwa hakitatoa mgombea urais katika uchaguzi ujao.

Tangazo hilo lilitolewa na viongozi wa PFF katika mkutano na waandishi wa habari, likieleza kuwa hatua hiyo inalenga kusaidia juhudi za upinzani kuungana na kuondoa utawala wa muda mrefu wa Rais Yoweri Museveni kwa njia ya mshikamano badala ya kugawanyika kwa wagombea wengi.

“Tumeamua kutotoa mgombea Urais mwaka 2026. Lengo letu ni kuhakikisha kuna mgombea mmoja wa upinzani kwa pamoja,” alisema Ibrahim Ssemuju Nganda, Katibu Mkuu wa chama cha PFF.

Wito wa umoja wa vyama vya upinzani

PFF tayari imesaini makubaliano ya ushirikiano na chama cha Alliance for National Transformation (ANT) kinachoongozwa na Jenerali mstaafu Mugisha Muntu, mwezi Julai 2025.

Mazungumzo pia yanaendelea kati ya PFF na chama cha National Unity Platform (NUP) kinachoongozwa na Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, kwa lengo la kupata mgombea mmoja kutoka upinzani kuelekea uchaguzi wa 2026.

Dkt. Kizza Besigye, ambaye tayari amewahi kugombea urais mara nne dhidi ya Rais Museveni bila mafanikio, hatagombea tena mwaka 2026.

PFF imeeleza kuwa sababu kuu za kutotoa mgombea ni pamoja na mazingira magumu ya kisiasa, kukamatwa na kuteswa kwa wanachama wa upinzani, pamoja na kile walichokiita “jeshi na familia kutawala nchi.”

“Tunalenga kujenga harakati ya wananchi kwa ajili ya mabadiliko ya kweli” Ssemuju amesisitiza.

InayohusianaTRT Afrika - Mwanasiasa Besigye wa Uganda arudishwa gerezani

 

CHANZO:TRT Arabi