Mahakama moja ya Kenya imetoa hati ya kukamatwa na kutaka raia mmoja wa Uingereza arejeshwe nchini humo (Kenya) ili akabiliwe na mashtaka ya mauaji ya mwanamke mwenye umri wa miaka 21 karibu na kambi ya mafunzo ya jeshi la Uingereza iliyoko Kenya, zaidi ya miaka kumi iliyopita.
Jaji Alexander Muteti wa Mahakama Kuu ya Nairobi alitangaza siku ya Jumanne kwamba kuna "sababu za msingi za kuamuru kukamatwa kwa mtuhumiwa" na akatoa hati ya kukamatwa kwa "raia mmoja wa Uingereza anayeishi Uingereza".
Kesi hiyo imekuwa chanzo cha mvutano kati ya Kenya na Uingereza, huku mataifa hayo yakibishana kuhusu mamlaka ya kisheria ya kuwashtaki wanajeshi wa Uingereza walioko nchini Kenya.
Agnes Wanjiru, ambaye alikuwa mama wa mtoto wa miezi minne wakati huo, alipatikana kuwa aliteswa kwa kupigwa na kuchomwa kisu, na huenda alikuwa bado hai alipokuwa akitupwa ndani ya tanki hilo la majitaka, kulingana na uchunguzi wa mahakama uliofanywa mwaka 2019.
Baada ya uamuzi wa Jaji Muteti, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) iliandika kwenye mtandao wa X kwamba “mchakato wa kurejesha mtuhumiwa nchini utaanza ili kuhakikisha anafikishwa mahakamani Kenya.”
ODPP iliongeza kuwa “kesi hiyo itarudi mahakamani tarehe 21 Oktoba 2025 kwa maelekezo zaidi.”
Dada wa Wanjiru, Rose Wanyua Wanjiku, mwenye umri wa miaka 52, alipokea uamuzi huo kwa furaha na kusema, “Haki ishinde.”
“Kwa familia yetu, tunafuraha sana kwa sababu imechukua miaka mingi, lakini sasa tunaona hatua imepigwa,” aliiambia shirika la habari la AFP.
Mpwa wa Wanjiru, Esther Njoki, naye aliiambia shirika la habari la Reuters kwamba ingawa wanakaribisha taarifa hiyo, imechukua muda mrefu mno.
“Tunashukuru kuona serikali ya Kenya imetenda, japo imechelewa sana na kutuacha gizani kama familia,” alisema Njoki.
Msemaji wa serikali ya Uingereza alikiri kuwa ODPP imeamua kuwa “raia mmoja wa Uingereza anapaswa kufikishwa mahakamani kuhusiana na mauaji ya Bi. Wanjiru mwaka 2012.”
Msemaji huyo aliongeza kuwa serikali ya Uingereza “imejitolea kikamilifu kusaidia Kenya kufanikisha upatikanaji wa haki.”