Bunge la Djibouti limeondoa ukomo wa umri kwa wagombea urais, na kufungua mlango kwa Ismail Omar Guelleh kuwania muhula wa sita ambapo wakati wa uchaguzi huo mwakani atakuwa na umri wa miaka 78.
Djibouti inatarajiwa kufanya Uchaguzi wa Urais Aprili 2026.
Wabunge wote 65 waliohudhuria walipiga kura Jumapili kuondoa kizuizi cha umri cha miaka 75.
Uamuzi huo utahitaji kuidhinishwa na rais pamoja na bunge kupiga kura nyingine Novemba 2, au kwa taifa kupiga kura ya maamuzi.
Guelleh ameongoza taifa hilo la Pembe ya Afrika tangu 1999, alipomrithi Hassan Gouled Aptidon, rais mwanzilishi wa nchi hiyo.
Ukomo wa umri ulianzishwa na Guelleh mwenyewe mnamo 2010 pamoja na mageuzi ambayo yaliondoa ukomo wa mihula ya rais, lakini ikapunguza kila muhula kutoka miaka sita hadi mitano.
Spika wa Bunge la Kitaifa Dileita Mohamed Dileita alitetea mabadiliko hayo kama muhimu kwa kudumisha uslama katika eneo lenye machafuko.
Alisema uungwaji mkono wa umma ulizidi asilimia 80 kwa hatua hiyo.
Mapema mwaka huu, katika mahojiano na jarida la Jeune Afrique, Guelleh alitoa ishara kwamba hakuwa na mpango wa kuachia madaraka.
"Ninachoweza kukuambia ni kwamba ninaipenda nchi yangu kupita kiasi hadi kuanza safari ya kutowajibika na kuwa sababu ya migawanyiko," alisema.
Watetezi wa haki wamelaani hatua hiyo kama ya kuelekea kuwa uongozini maisha
Guelleh alishinda muhula wake wa tano mwaka 2021 kwa zaidi ya asilimia 98 ya kura baada ya miungano ya upinzani kususia uchaguzi huo.














