Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imetuma waangalizi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania.
“ Kutumwa kwa ujumbe huo kunatokana na mualiko wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ni kwa kuzingatia agizo la Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki linaloitaka Sekretarieti hiyo kusimamia uchaguzi katika Nchi zote Washirika.” EAC ilisema katika taarifa.
Mkuu wa ujumbe huo ni Dkt. Specioza Wandira Kazibwe, makamu wa Rais wa zamani wa Uganda (1994–2003).
"Kama Jumuiya iliyosimikwa katika misingi ya utawala bora, utawala wa sheria, na kuheshimu haki za binadamu, EAC inaona uchaguzi unaoaminika kuwa msingi wa demokrasia na mtangamano wa kikanda," Dkt. Kazibwe alibainisha.
Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa EAC unajumuisha waangalizi 67 kutoka nchi zote Wanachama wa EAC, wakiwemo wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), wawakilishi wa Tume za Taifa za Uchaguzi, Tume za Kitaifa za Haki za Binadamu, asasi za kiraia na Sekretarieti ya EAC.
“ Waangalizi wamechaguliwa kwa uangalifu kwa utaalamu wao, kutopendelea, na kujitolea kwa maadili ya Jumuiya.” EAC imesema.
Waangalizi hao walitumwa rasmi katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania ili kutathmini mwenendo wa mchakato wa uchaguzi.
"Majukumu yao ni kutathmini uchaguzi kwa kuzingatia sheria za kitaifa, Kanuni za EAC za Uangalizi na Tathmini ya Uchaguzi, na viwango husika vya kimataifa," Dk. Kazibwe alieleza.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Veronica Nduva, alibainisha kuwa Ujumbe huo utatoa taarifa ya awali muda mfupi baada ya uchaguzi huo, ikifuatiwa na ripoti ya mwisho ya kina.
"Ripoti hizi zitawasilisha matokeo yetu na kutoa mapendekezo yanayolenga kuimarisha michakato ya uchaguzi katika eneo hili," alisema.
Wakati huo huo Jeshi la Polisi Tanzania (TPF) lilitoa taarifa kwa Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya usalama na hali ya kujipanga kwa polisi kuelekea Uchaguzi Mkuu.













