Lazarus Chakwera, ‘Baba Mchungaji’ wa Malawi aliyekubali kushindwa uchaguzi
Rais wa Malawi anayemaliza muda wake, Lazarus Chakwera./Picha:Wengine
Lazarus Chakwera, ‘Baba Mchungaji’ wa Malawi aliyekubali kushindwa uchaguzi
Alijipenyenza kwenye siasa akiwa kama kiongozi wa chama cha upinzani cha Malawi Congress Party (MCP), ambacho kilihusika na kuuangusha utawala wa Kiingereza mwanzoni mwa miaka ya 60.
26 Septemba 2025

Anaitwa Lazarus Chakwera, ama ukipenda muite Lazaro, kama yule wa kwenye Biblia.

Huyu ni rais wa Malawi, aliyemaliza muhula wa kwanza wa uongozi wake, huku rais wa zamani wa nchi hiyo Peter Mutharika akionesha kuonesha kuongoza katika matokeo ya awali ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni.

Akiwa amezaliwa Aprili 5, 1955, Rais Chakwera alitumia muda mrefu wa maisha yake kama mwanateolojia na kwa nyakati tofauti amehudumu kama ‘baba mchungaji’ kabla ya kuingia kwenye ulingo siasa za Malawi mwaka 2013.

Alijipenyenza kwenye siasa akiwa kama kiongozi wa chama cha upinzani cha Malawi Congress Party (MCP), ambacho kilihusika na kuuangusha utawala wa Kiingereza mwanzoni mwa miaka ya 60.

Ikumbukwe kuwa, Baba Mchungaji Chakwera aliwania kiti cha urais mara mbili, mwaka 2014 na 2019, akishika nafasi ya pili kwa nyakati mbalimbali.

Akishirikiana na aliyekuwa mgombea mwenza wake Saulos Chilima, Chakwera, aliongoza Umoja wa Tonse, ambao uliundwa na vyama tisa vya upinzani, kuondoa madarakani utawala wa rais Mutharika.

Wakati akiwania nafasi ya urais, Chakwera alijinasibu kuwa yeye ni mtumishi wa watu, aliyeazimia kuunganisha Wamalawi wote, kukomesha ufisadi na kukuza uhuru wa mahakama na utawala wa sheria.

Hata hivyo, miaka mitano baadaye, mambo hayajenda kama alivyopanga, huku raia wa Malawi wakihisi kuwa ‘Baba Mchungaji’ amewaangusha, na ni wakati muafaka wa kumpumzisha, wakihisi kwamba, bora jini likujualo kwani halikuli likakumaliza.

CHANZO:TRT Afrika Swahili