Polisi walifyatua gesi ya kutoa machozi kuwatawanya maelfu ya waandamanaji, wengi wao wakiwa vijana, waliokuwa wakitembea mitaani na mabango katika jiji la Antananarivo, mji mkuu wa nchi hiyo, mmoja wa wakazi aliliambia Shirika la habari la Reuters.
Waandamanaji walikuwa wakilalamikia serikali na kuitaka irejeshe huduma ya kuaminika ya maji na umeme nchini kote.
“Kuna watu wachache wanaotumia fursa hii kuharibu mali za wengine,” alisema Jenerali Angelo Ravelonarivo, kiongozi wa kikosi cha usalama cha pamoja kinachojumuisha polisi na jeshi, katika taarifa aliyoisoma kupitia televisheni ya Real TV, Alhamisi usiku.
Ili kulinda "wananchi na mali zao," vyombo vya usalama viliamua kuweka amri ya kutotoka nje kuanzia saa 1 jioni hadi saa 11 alfajiri “hadi hali ya usalama itakaporejea,” taarifa hiyo ilisema.
Madagascar, taifa lililoko katika Bahari ya Hindi, linakabiliwa na umasikini mkubwa, na baadhi ya raia wanailaumu serikali ya Rais Andry Rajoelina, kwa kushindwa kuboresha hali ya maisha. Rajoelina alichaguliwa tena mwaka 2023.
Wakati wa maandamano hayo siku ya Alhamisi, jumba kubwa la biashara jijini lilivunjwa na watu kuibwa, na baadae kulichoma moto. Pia, nyumba za wabunge wawili zilivunjwa na kuharibiwa, kwa mujibu wa shahidi huyo wa Reuters.
Waandamanaji, ambao walikaidi marufuku ya awali ya polisi kuhusu maandamano hayo, walikuwa wakipiga kelele na kusema: “Tunataka maji, tunataka umeme.”
Baada ya maandamano hayo kutawanywa, yaliendelea kusambaa hadi katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Msemaji wa vyombo vya usalama, Zafisambatra Ravoavy, hakupatikana kutoa maoni.
Siku ya Jumatano, Mkuu wa Polisi wa Taifa, Jean Herbert Andriantahiana Rakotomalala, alionya kuwa vyombo vya usalama “vitachukua hatua kali dhidi ya wale wanaojaribu kuvunja sheria.”