Gavana wa Darfur, ambaye anaunga mkono jeshi la Sudan, ametoa wito wa “kulindwa kwa raia” katika mji wa El-Fasher unaokabiliwa na njaa kali, baada ya wapiganaji wa RSF kudai kuwa wamedhibiti eneo hilo.
RSF imekuwa ikipigana vita vikali na jeshi la Sudan tangu Aprili 2023.
“Tunataka kulindwa kwa raia, kufichuliwa kwa hatma ya wakimbizi wa ndani, na kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu na mauaji ya halaiki yanayotekelezwa na wanamgambo hawa kwa siri,” alisema Gavana Minni Minnawi siku ya Jumatatu.
Kundi la Madaktari wa Sudan liliongeza kuwa RSF inawaua raia kwa misingi ya kikabila na kuvamia vituo vya afya katika El-Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini, magharibi mwa Sudan.
Mji uliozingirwa
“Katika tukio la mauaji ya kikatili yaliotekelzwa na RSF jana jioni mjini El-Fasher — yakiwa ni mwendelezo wa uhalifu wao katika El-Fasher na eneo zima la Darfur — RSF iliua raia wasio na silaha kwa misingi ya kikabila,” ilisema taarifa ya Kundi la Madaktari wa Sudan kupitia mtandao wa kijamii X (zamani Twitter) siku ya Jumatatu.
“Tunaendelea kukabiliwa na ugumu wa kufika katika maeneo yaliyoathirika kutokana na hali ya usalama iliyoporomoka kabisa iliyosababishwa na RSF,” taarifa hiyo iliongeza.
Kwa wiki kadhaa sasa, El-Fasher imekuwa uwanja wa mapigano makali kati ya jeshi la Sudan na RSF, kufuatia shambulio la pande nyingi lililoanzishwa na wanamgambo hao waliouzunguka mji huo kutoka pande tano kwa lengo la kuuteka kutokana na umuhimu wake wa kimkakati.
RSF imeizingira mji wa El-Fasher tangu Mei 10, 2024, huku jeshi la Sudan likijaribu kuuvunja mzingiro huo. Mji wa El-Fasher ni kituo kikuu cha shughuli za kibinadamu kwa majimbo yote matano ya Darfur.














