Rais wa Cameroon Paul Biya amechaguliwa tena kwa muhula wa nane ambao huenda ukamuweka madarakani hadi karibu miaka 100, kulingana na matokeo rasmi yaliyotangazwa siku ya Jumatatu na Baraza la Kikatiba la nchi hiyo ya Afrika ya Kati.
"Natangaza hapa Rais-mteule: mgombea Biya Paul," alisema Clement Atangana, rais wa Baraza la Katiba.
Biya, mwenye umri wa miaka 92, aliingia madarakani 1982 na ameshikilia madaraka tangu wakati huo, kwa kuondoa ukomo wa mihula ya rais 2008 na kushinda mara kwa mara mihula kwa kishindo.
Mwaka huu upinzani mkali ulitoka kwa Issa Tchiroma Bakary, aliyekuwa msemaji wa serikali na waziri wa ajira ambaye ana miaka zaidi ya sabini na alitofautiana na Biya mapema mwaka huu na kuendesha kampeni ambazo zilivutia watu wengi kwenye mikutano pamoja na kuungwa mkono na miungano ya vyama vya upinzani na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.














