AFRIKA
2 dk kusoma
Raia wa Tanzania wapiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2025
Raia wa Tanzania kutoka sehemu mbalimbali za nchi wameanza kupiga kura mapema hii. Zoezi hilo limeanza rasmi saa moja asubuhi na linatarajiwa kukamilika saa kumi alasiri.
Raia wa Tanzania wapiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2025
Tanzania elections / TRT Afrika Swahili
tokea masaa 15

Na Abubakar Famau akiwa Dodoma

Watanzania kutoka sehemu mbalimbali za nchi wameanza kupiga kura mapema hii. Zoezi hilo limeanza rasmi saa moja asubuhi na linatarajiwa kukamilika saa kumi alasiri.
TRT Afrika, ambayo imekita kambi jijini Dodoma imeshuhudia zoezi hilo likiendelea kwa utulivu, ingawa mwitikio unaonekana kuwa mdogo ikilinganishwa na uchaguzi uliopita.

Tume ya uchaguzi nchini humo inatarajia wapiga kura milioni 37 kujitokeza na kuchagua viongozi wao katika ngazi ya urais, ubunge na udiwani.Baadhi ya wananchi waliojitokeza asubuhi hii na kufanikiwa kupiga kura ni Mohammed Yassin Aziz mkazi wa Dodoma ambae anasema kuwa amefurahi kufanikiwa kupiga kura."

Zoezi limeenda vizuri bila bughudha yoyote. Hii ni mara yangu ya nne kupiga kura. Kwa sasa hivi muitikio sio mzuri tofauti na uchaguzi uliopita ambapo foleni zingekuwa ndefu zaidi," anasema Mohammed.Hata hivyo, kwa Emmanuel Elias ambae aliwahi kufika katika kituo cha Jumba la Maendeleo kituo namba tatu kilichopo katika Kata ya Uhuru kilichopo Dodoma mjini baada ya kushindwa kupiga kura kutokana na taarifa zake kutokuwepo."

Nimekuja kupiga kura kwa sababu ni haki yangu. Ila nimejisikia vibaya jina kukosekana, ila bado nina matumaini," anasema Emmanuel.Kwa Asia Juma Abdallah siku hii amekuwa akiisubiri kwa hamu kwani anasema kuwa amefurahishwa kuona wanawake wengi wameshiriki katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa mwaka huu."Mimi ni mzalendo nimeamka asubuhi na mapema kuja kumchangua nimtakae. Hakuna usumbufu wowote uliojitokeza.

Ninaipongeza Tume ya Uchaguzi kwa maandalizi mazuri yaliyofanyika," amesema Asia pindi alipozungumza na TRT Afrika.Wachambuzi wa masuala ya siasa nchini Tanzania wanasema uchaguzi wa mwaka huu unaweza kukosa muitikio ikilinganishwa na uchaguzi uliotangulia hasa baada ya kuzuka hofu ya kuwepo kwa maandamano yaliyoitishwa wa wanaharakati mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii, kwa lengo la kudai mabadiliko.

Jumla ya vyama 17 vina wagombea urais pamoja na wagombea wenza wao. Tume Huru ya Uchaguzi nchini Tanzania imesema matokeo ya urais yatakuwa wazi ndani ya saa 72 baada ya upigaji kura kukamilika huku Mwenyekiti wa Tume hiyo akisema kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu, uimarishaji mkubwa umefanyika wa kimfumo hivyo kuongeza ufanisi wa utendaji.