Tanzania: Watumishi wa umma na wanafunzi kubaki nyumbani baada ya vurugu za siku ya Uchaguzi
Waandamanaji walipambana na polisi na ofisi ya serikali ya mtaa ikachomwa moto jijini Dar es Salaam. Huduma ya mtandao ilitatizwa kote nchini.
Tanzania: Watumishi wa umma na wanafunzi kubaki nyumbani baada ya vurugu za siku ya Uchaguzi
Uchaguzi Mkuu Tanzania ulifanyika 29 Oktoba 2025 / Reuters
tokea masaa 12

Serikali ya Tanzania imewaagiza watumishi wa umma na wanafunzi kubaki nyumbani siku ya Alhamisi, siku moja baada ya uchaguzi mkuu uliokumbwa na maandamano ya vurugu kusababisha polisi kutangaza amri ya kutotoka nje jijini Dar es Salaam.

Waandamanaji waliingia barabarani katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam na miji mingine kadhaa wakati wa upigaji kura siku ya Jumatano, wakieleza kukasirishwa na kutengwa kwa wapinzani wakuu wawili wa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kinyang'anyiro cha Urais, pamoja na kile wanachosema ni kuzidisha ukandamizaji kwa wakosoaji wa serikali.

Waandamanaji walikabiliana na polisi. Ofisi ya serikali za mitaa ilichomwa moto jijini Dar es Salaam. Huduma ya mtandao ilitatizwa kote nchini.

"Watumishi wote wa umma nchini wanatakiwa kufanyia kazi wakiwa nyumbani isipokuwa wale ambao majukumu yao ya kazi yanawahitaji wawepo katika maeneo yao ya kazi kama wanavyoelekezwa na waajiri wao," ilisema taarifa iliowekwa kwenye akaunti ya Instagram ya msemaji wa serikali Gerson Msigwa Jumatano jioni.

Kituo cha televisheni cha serikali pia kilitangaza kwamba wanafunzi wanatakiwa kusoma kutoka nyumbani siku ya Alhamisi.

Msigwa hakujibu simu wala ujumbe mfupi wa simu kufafanua kuhusu suala hilo.

Mitaa ya Dar es Salaam ilikuwa tulivu mapema siku ya Alhamisi huku baadhi ya wakazi wakikiuka amri ya kutotoka nje, na maafisa wa usalama wakishika doria mitaani.

Lakini kwenye programu ya Zello, ambayo inaruhusu simu janja kufanya kazi kama ‘‘walkie-talkie’’, baadhi ya waandamanaji walijadili mipango ya maandamano zaidi, ikiwa ni pamoja na maandamano katika maeneo ya majengo ya serikali.

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA kilitoa wito wa maandamano wakati wa uchaguzi huo, ambao walisema ni sawa na "kutawazwa" kwa Rais Samia.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilienguliwa mwezi Aprili katika uchaguzi huo ambao pia ulijumuisha kura za wabunge na wawakilishi wa visiwani Zanzibar, baada ya kukataa kusaini kanuni za maadili na kiongozi wake Tundu Lissu kufunguliwa mashtaka ya uhaini.

Tume hiyo pia ilimwondolea sifa mgombea wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, huku ikiacha vyama vidogo tu kugombea dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Samia, mmoja wa wakuu wawili wa nchi wanawake barani Afrika, alipata sifa baada ya kuchukua madaraka mwaka 2021 na kuondoa kile kilichoonekana kuwa ukandamizaji wa wapinzani wa kisiasa chini ya mtangulizi wake John Pombe Magufuli.

Katika miaka ya hivi karibuni, hata hivyo, wanaharakati wa haki za binadamu na wagombea wa upinzani wameishutumu serikali kwa utekaji nyara wa wakosoaji wake.

Rais Samia alisema mwaka jana aliagiza uchunguzi ufanyike kuhusu taarifa za utekaji nyara. Hakuna matokeo rasmi ambayo yametolewa kwa umma.

CHANZO:TRT Afrika and agencies