Watanzania wamepiga kura 29 Oktoba 2025, katika uchaguzi ambao Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kushinda baada ya wagombea wa vyama viwili vikuu vya upinzani kuzuiwa kugombea.
Mbali na uchaguzi wa rais, wapiga kura wanachagua wabunge wa bunge la Jamhuri, visiwani Zanzibar ambayo ina mamlaka yake wanachagua rais na wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi.
Kura hiyo inafanyika bila ushiriki wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA ambacho kiongozi wake Tundu Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini jambo ambalo amelikanusha.
Tume ya uchaguzi iliiondoa CHADEMA mwezi Aprili baada ya chama hicho kukataa kutia saini kanuni ya maadili ya uchaguzi.

Tume hiyo pia imemuengua mgombea urais kwa tiketi ya chama cha pili kwa ukubwa cha upinzani ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina baada ya pingamizi kutoka kwa mwanasheria mkuu wa serikali na kuwaacha wagombea wa vyama vidogo pekee kukabiliana na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Samia Suluhu Hassan.
"Hakuna uchaguzi nchini Tanzania. Ikiwa naweza kuweka mtazamo sahihi, ni kutawazwa," Deogratias Munishi, Katibu wa CHADEMA anayeshughulikia masuala ya Mambo ya Nje, aliiambia Televisheni ya Citizen katika nchi jirani ya Kenya Jumatano.
Idadi ya watu waliojitokeza mapema ilionekana kuwa ndogo katika vituo vya kupiga kura kwenye mji mkuu wa kibiashara wa Dar es Salaam, ambako hakukuwa na dalili zozote za maandamano ambayo baadhi ya wanaharakati walikuwa wameitisha kwenye mitandao ya kijamii.
Rais Samia aliwaambia waandishi wa habari baada ya kupiga kura katika mji mkuu wa Dodoma:
"Nawaomba Watanzania wote, wale ambao bado wako nyumbani, wajitokeze kutekeleza haki yao na kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowapenda." Alisema Rais Samia.
Juma Mtali, mfanyabiashara aliyepiga kura jijini Dar es Salaam, aliiambia Reuters kwamba kwakwe zoezi limekuwa zuri.
“Vijjana walikuwa wametoa wito wa maandamano wakati wa uchaguzi huu lakini kwa sasa ni wa amani,” alisema. "Kila kitu kinakwenda vizuri sana."
Chama cha Rais Samia Suluhu Hassan, CCM ambacho kimekuwa uongozini kikirithi kile kile cha TANU wakati wa harakati za kupata uhuru, kimekuwa kwenye uongozi wa nchi hiyo kwa muda wote.
Ikirejelea ukosoaji kutoka kwa mashirika mengine ya haki na takwimu za upinzani, Amnesty International wiki iliyopita ilishtumu mamlaka kwa kukandamiza upinzani. Serikali ilikanusha shutma hizo na imesema uchaguzi unaendeshwa kwa haki na kwa mujibu wa sheria.
Tume ya uchaguzi inasema itatangaza matokeo ya Urais ndani ya siku tatu baada ya kumalizika kwa kupiga kura. Upiganji kura ulianza saa moja asubuhi na vituo vitafungwa saa kumi jioni.
Samia, ambaye mabango yake yako katika kila maeneo ya miji na vijijini, amefika katika mengi nchini humo akiomba kura kwa taifa hilo lenye watu zaidi ya milioni 68.
Amejivunia upanuzi wa ujenzi wa barabara na reli na kuongeza uwezo wa kufua umeme. Katika muhula wake ujao, ameahidi kulipa kipaumbele suala la kuajiri walimu zaidi.
Samia alisifiwa baada ya kuingia madarakani mwaka 2021 kwa kuwapa nafasi wapinzani wa kisiasa, ambao hawakuwa na fursa hiyo wakati wa mtangulizi wake, John Pombe Magufuli, aliyefariki akiwa madarakani.
Lakini katika miaka miwili iliyopita, wanaharakati wa haki za binadamu na wanachama wa upinzani wameishutumu serikali kwa matukio ya utekaji wa wakosoaji wake.
Rais Samia, mmoja wa viongozi wa nchi wanawake wawili barani Afrika, amesema serikali yake imejitolea kuheshimu haki za binadamu na mwaka jana aliamuru uchunguzi ufanyike kuhusu ripoti za utekaji nyara.
Hakuna matokeo rasmi ambayo yametolewa kwa umma.











