Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty, ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano kwa misingi ya kibinadamu nchini Sudan kufuatia ripoti za ukatili unaotekelezwa na wanamgambo wa RSF katika mji wa Al Fasher, magharibi mwa nchi hiyo.
Wito huo umetolewa Jumatano mjini Cairo wakati wa kikao kati ya Abdelatty na waziri mwenzake wa Sudan, Mohieddin Salem Ahmed, kujadili hali ya Al Fasher — makao makuu ya jimbo la Kaskazini mwa Darfur — ambayo ilitekwa na RSF siku ya Jumapili.
Abdelatty alisisitiza umuhimu wa kusitisha mapigano kwa jumla ili kuruhusu kufikishwa kwa misaada ya kibinadamu na kupunguza mateso ya raia.
Wizara ya mambo ya nje ya Misri ilisema katika taarifa kuwa waziri “alithibitisha uungaji mkono kamili wa Misri kwa watu wa Sudan na dhamira ya nchi hiyo kuendelea kujitahidi kurejesha amani na uthabiti Sudan.”
Mauaji ya dhulma
Siku ya Jumanne, mataifa ya Kiarabu na mashirika ya kikanda yalilaani vikali dhidi ya kile walichokiita “uvunjaji mkubwa wa haki za kibinadamu” unaotekelezwa na RSF katika mji wa Al Fasher.
Mamlaka za Sudan na mashirika ya kimataifa yameishutumu RSF kwa kufanya “mauaji ya halaiki na ukiukaji wa haki za kibinadamu” katika Al Fasher, ikiwemo “mauaji ya dhulma,” kukamatwa kiholela, na kuwahamisha raia kwa nguvu wakati wa uvamizi wao katika mji huo uliokuwa umezingirwa kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Tangu Aprili 15, 2023, jeshi la Sudan na RSF wamekuwa wakipigana vita ambavyo juhudi nyingi za upatanisho wa kikanda na kimataifa zimeshindwa kuvimaliza.
Mgogoro huo umesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwafanya zaidi ya watu milioni 15 kukimbia makazi yao.











