Idadi ya wagonjwa wa kipindupindu waliosajiliwa inaongezeka, huku zaidi ya watu 4,200 wakifariki kutokana na ugonjwa huo barani Afrika mwaka 2025, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limesema siku ya Alhamisi.
Patrick Abok, Kaimu Mkurugenzi wa dharura wa kanda katika Ofisi ya WHO Kanda ya Afrika, alisema kanda hiyo inakabiliwa na hali ya dharura ya afya katika miaka ya hivi karibuni.
Alitoa mfano wa mlipuko mpya wa Ebola katika jimbo la Kasai la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kipindupindu, Mpox, surua na magonjwa mengine ambayo yanaendelea kusumbua mfumo wa afya ambao tayari ni dhaifu.
"Mwaka huu pekee, zaidi ya watu 190,000 wameambukizwa ugonjwa wa kipindupindu na zaidi ya 4,200 wamekufa kutoka nchi 23, ambapo 16 bado wana milipuko inayoendelea," Abok alisema katika mkutano wa wanahabari kutoka Angola, ulioitishwa kuwajulisha waandishi wa habari juu ya dharura za kiafya za kanda.
"Upatikanaji wa maji salama na vifaa vya usafi bado hautoshi, na kwa hivyo kipindupindu kinaendelea kuwa hatari kubwa kwa afya ya umma katika maeneo ambayo tayari yanakabiliwa na janga la kibinadamu."
Abok alisema WHO inasaidia vituo vya matibabu ya kipindupindu, kutoa vifaa na kuwezesha chanjo ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo - na zaidi ya dozi milioni 15 zimetolewa mwaka huu.
Ugonjwa wa kipindupindu umekumba mataifa kadhaa ya Afrika, zikiwemo Chad, Sudan, Ethiopia, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kutokana na hali duni ya usafi wa mazingira na mafuriko yanayohusiana na hali ya hewa.
Maambukizi ya bakteria husababishwa na ulaji wa maji au chakula kilichochafuliwa.