Hakukuwa na watu katika barabara za mji mkuu wa Madagascar siku ya Ijumaa huku wakaazi wakikadiria hasara baada ya maandamano ya vurugu kuhusu kukatwa mara kwa mara kwa umeme na uhaba wa maji.
Maandamano katika mji wa Antananarivo, yakiongozwa na mamia ya vijana, yalikabiliwa na polisi, waliorusha risasi za mpira pamoja na mabomu ya machozi ili kuwatawanya waandamanaji.
Vurugu hizo ziliendelea hadi usiku, kulazimisha polisi kutangaza marufuku ya kutotoka nje kuanzia jioni hadi alfajiri baada ya kutokea uporaji katika mabenki na maduka kuchomwa moto. Nyumba za wabunge watatu wa upande wa serikali pia zilichomwa moto.
Hakukuwa na polisi wengi
Wakaazi walioshtushwa - wengine wakiwa wanalia - walitathmini hasara waliyopata Ijumaa asubuhi, mwandishi wa habari wa AFP aliyekuwepo kwenye eneo la tukio alieleza.
Hakukuwa na polisi wengi katika medani ya mji mkuu tofauti na ilivyokuwa siku ya Alhamisi, ambapo maafisa wa polisi walikuwa wanashika doria wakizuia waandamanaji kukusanyika.
Asubuhi iliyofuata magari yakarudi tena katikati mwa mji, ingawa idadi ilikuwa ndogo.
Huku hali ikiwa imetulia mjini, kulikuwa na taarifa za uporaji katika sehemu nyingine ya Antananarivo.
Hasira za watu
Waandamanaji walieleza hasira zao kuhusu kukatwa kwa umeme mara kwa mara na uhaba wa maji, ambao unatatiza biashara za watu na kuacha nyumba bila umeme kwa zaidi ya saa 12 kwa siku kote nchini.
Nchi hiyo ya Bahari Hindi inaongoza kwa uzalishaji wa vanilla, moja ya viungo ghali baada ya zafarani.