AFRIKA
2 dk kusoma
Samia: Tutajenga barabara ya tabaka gumu kati ya Ngorongoro na Serengeti
Ni mwezi mmoja tu umesalia, kabla ya Watanzania kufanya uchaguzi wa Madiwani, Wabunge na Rais.
Samia: Tutajenga barabara ya tabaka gumu kati ya Ngorongoro na Serengeti
Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM./Picha:@ccm_tanzania
3 Oktoba 2025

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema endapo ataaminiwa na Watanzania kuunda serikali, atahakikisha wilaya za Ngorongoro na Monduli zinaunganishwa kwa kiwango cha lami, sanjari na ujenzi wa barabara ndani ya wilaya hizo ili kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi.

Akizungumza Ijumaa ya Oktoba 3, 2025 jijini Karatu mkoani Arusha, Samia amesema usanifu wa barabara ya Engaruka–Ngaresero yenye urefu wa kilomita 24 umekamilika na serikali ipo katika hatua za kutangaza zabuni.

Aidha, ametaja barabara ya Selela–Engaruka yenye urefu wa kilomita 17 kuwa ipo kwenye maandalizi ya zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi atakayejenga barabara hiyo muhimu, ambayo itaunganishwa na kiwanda cha magadi soda na kutumika pia kwa shughuli za utalii katika Ziwa Natron, wilayani Monduli.

Kwa upande wa Karatu, Dkt. Samia ameahidi ujenzi wa barabara ya kutoka Geti la Ngorongoro kuelekea Serengeti yenye urefu wa kilomita 88, itakayojengwa kwa tabaka gumu katika awamu tatu, ambapo awamu ya kwanza itagharimu shilingi bilioni 70 na ujenzi wake unatarajiwa kuanza katika mwaka huu wa fedha.

Pia ameahidi kufanyia kazi ombi la wananchi kuhusu ujenzi wa kilomita 10 za barabara zinazoelekea kwenye hoteli za watalii wilayani Karatu, pamoja na kufunga taa za barabarani kuanzia eneo la Mto wa Mbu hadi Karatu Mjini na kuendelea hadi kwenye geti la hifadhi ya Ngorongoro.

Ni mwezi mmoja tu umesalia, kabla ya Watanzania kufanya uchaguzi wa Madiwani, Wabunge na Rais.

CHANZO:TRT Afrika Swahili