ACT Wazalendo Zanzibar yataka uchaguzi sawa na wa haki
Othman amesema kuwa serikali yake haitoruhusu biashara ama uwekezaji kwa wageni unaoweza kufanywa na wenyeji na badala yake itawezesha wananchi kiutalamu.
ACT Wazalendo Zanzibar yataka uchaguzi sawa na wa haki
Othman Masoud Othman, mgombea urais Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo. Picha/ACT Wazalendo / TRT Afrika Swahili
7 Oktoba 2025

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo Othman Masoud Othman amesema kuwa uchaguzi wa wizi na ghilba unaweza kuirudisha Zanzibar ilipotoka baada ya juhudi kubwa za kuasisi Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Othman ambae pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, ameyasema hayo akiwa katika viwanja vya Avenger Jimbo la Chumbuni  wilaya ya Mjini Unguja katika mkutano wa hadhara alipokuwa akifanya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.

Othman ameongeza kusema kuwa, kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ilitokana na hekma na juhudi kubwa za watangulizi katika kustawisha amani ya kweli  Zanzibar na kwamba ni vyema  nchi ifanye uchaguzi wa haki na usawa.

Aidha amesema kwamba iwapo atashinda urais, serikali yake haitoruhusu biashara ama uwekezaji kwa wageni unaoweza kufanywa na wenyeji na badala yake itawezesha wananchi kiutalamu, nyenzo na rasilimali ili waweze kufanya shughuli hizo na kuwapatia ajira na kipato chenye manufaa.