Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imetangaza kuwa jumla ya wapiga kura 717,557 ndiyo waliodhinishwa kushiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mara baada ya kukamilika kwa mchakato wa uhakika wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Kulingana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ZEC, Thabit Idarous Faina, jumla ya wapiga kura 8,325 wameondolewa katika daftari hilo kutokana na kukosa sifa.
Kati ya wapigakura waliodhinishwa, wanawake ni 378,334, ambayo ni sawa na asilimia 53, huku wanaume wakiwa 339, 223, sawa na asilimia 47.
Kati ya idadi hiyo, vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 ni 326,304(asilimia 45), wenye umri wa miaka 36 hadi 59 ni 300,986(asilimia 42) na walio na umri wa miaka 59 na kuendelea ni 90,267 ambayo ni sawa na asilimia 13.
“Hii ndiyo nguvu ya kisiasa iliyo mbele yenu, Ni wajibu wenu wanasiasa kufahamu namna ya kuwafikia wapigakura hawa ili kuwashawishi katika kampeni,”alisema Faina, wakati wa mkutano na wadau wa uchaguzi visiwani humo.
Wakati uchaguzi wa Tanzania bara ukisimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), uchaguzi wa Zanzibar unasimamiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Tanzania Bara ina jumla ya wapiga kura milioni 36,929,683. Hii ni ongezeko la wapiga kura milioni 7.9 sawa na asilimia 26.6 toka wapiga kura milioni 29,754,696 waliosajiliwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.