AFRIKA
2 dk kusoma
Samia: CCM itajenga na kuinua utu wa Mtanzania
Kulingana na mgombea huyo, endapo CCM itapewa ridhaa ya kuongoza tena, serikali yake itaanza utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kila Mtanzania awe na uhakika wa matibabu bila hofu ya gharama.
Samia: CCM itajenga na kuinua utu wa Mtanzania
Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan./Picha:@ccm_tanzania
30 Septemba 2025

Mgombea wa Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amesema dhamira ya chama hicho ni kuendelea kujenga na kuinua utu wa Mtanzania kupitia miradi ya maendeleo na sera zinazogusa maisha ya kila mwananchi.

Akihutubia wananchi wa wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro Septemba 30, 2025, Rais Samia amesema CCM imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha huduma muhimu za jamii zinawafikia Watanzania wote, hususan vijijini.

“Tunapopeleka maji vijijini, tunapopeleka umeme vijijini, huduma za afya karibu na wananchi, elimu karibu na wananchi, kuzuia wanyama waharibifu wasile mazao na kutafuta masoko ya mazao yetu — huko ni kujenga utu wa Mtanzania,” amesema Samia, akibainisha kuwa hatua hizo zinaboresha maisha ya wananchi na kuongeza kipato.

Ameongeza kuwa endapo CCM itapewa ridhaa ya kuongoza tena, serikali yake itaanza utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kila Mtanzania awe na uhakika wa matibabu bila hofu ya gharama.

“Tumeshafanya kazi kubwa ya kusogeza huduma za afya karibu na wananchi. Kilichobaki sasa ni kuhakikisha mwananchi anatibiwa bila hofu. Ukilazwa, unatibiwa; hata kama bahati mbaya ukifariki, bima yako inakulipia. Huko ndiko kulinda na kuuenzi utu wa Mtanzania,” amesisitiza.

Samia amesema CCM inayoomba ridhaa ya kuendelea kuongoza ina wagombea mahiri kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani, na lengo ni kuhakikisha kila mwananchi ananufaika moja kwa moja na sera na miradi ya chama hicho.

CHANZO:TRT Afrika Swahili