AFRIKA
2 dk kusoma
Mahakama ya Tanzania yatupilia mbali hoja ya ACT Wazalendo
Katika utetezi wake, mahakama hiyo imesisitiza kwamba, hakuna ushahidi kuwa INEC imeanza kuchapisha karatasi hizo, zikiwa zimebakia siku 28 kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu nchini humo.
Mahakama ya Tanzania yatupilia mbali hoja ya ACT Wazalendo
Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu./Picha:TRTAfrikaswahili / TRT Afrika Swahili
29 Septemba 2025

Mahakama kuu ya Tanzania(Masjala Kuu ya  Dodoma) imetupilia mbali hoja iliyowasilishwa na Chama cha ACT Wazalendo ya kuiomba mahakama hiyo kuweka zuio la muda kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (INEC) kuendelea na mchakato wa uchapishaji wa karatasi za kura za wagombea wa nafasi za Urais nchini Tanzania.

Chama hicho, kiliomba mahakama hiyo, kuweka zuio hilo mpaka pale uamuzi wa shauri hilo litakapofanyika, hatua ambayo taasisi hiyo ya sheria, kudai kuwa haina msingi wowote.

Katika utetezi wake, mahakama hiyo imesisitiza kwamba, hakuna ushahidi kuwa INEC imeanza kuchapisha karatasi hizo, zikiwa zimebakia siku 28 kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu nchini humo.

Awali, upande wa serikali uliweka pingamimizi jingine likisema kwamba,  Mahakama Kuu haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza shauri hili la kumrudisha kwenye orodha ya wagombea wa nafasi ya Urais Luhaga Joelson Mpina.

Hata hivyo, Mahakama imeamua kwamba Shauri hilo la Kikatiba namba 24027 la mwaka 2025 lililofunguliwa na Mpina na Bodi ya Wadhamini ya chama hicho kupinga kitendo cha kuondolewa kwa mgombea Urais huyo kwenye Uchaguzi Mkuu litarushwa mubashara ili kutoa nafasi ya wananchi kufuatilia na kusikia hoja zinazowasilishwa na pande zote.

Hata hivyo, chama hicho cha upinzani kimesema kuwa bado hakijapoteza matumaini ya kuwa na mpina kama mpeperushaji bendera wao, wakati wa mchakato wa uchaguzi utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

“Sisi tunaamini hata ikibaki siku moja Mpina anaweza kukinadi chama chetu,” alisema Dorothy Semu, ambaye pia ni kiongozi wa ACT-Wazalendo, katika mahojiano yake na TRT Afrika.

Semu alisema kuwa bado ana amini kuwa Mahakama itatenda haki katika shauri hilo, huku akiongeza kwamba muda uliosalia bado unatosha kwa mgombea wao kuingia kwenye mchakato wa kampeni za Urais.

Mpina aliondolewa kwenye kinyang’anyiro hicho na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, INEC September 15 mwaka huu, baada ya kuwekewa pingamizi.

CHANZO:TRT Afrika Swahili