AFRIKA
2 dk kusoma
Samia: Wananchi tukapige kura usalama ni mkubwa
Kulingana na Samia, wale wanaoshawishi kuvunja amani wana mahali pa kukimbilia wao na familia zao.
Samia: Wananchi tukapige kura usalama ni mkubwa
Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan./Picha:@ccm_tanzania
1 Oktoba 2025

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wanachama wote wa chama hicho na Watanzania kwa ujumla wajitokeze kwa wingi Oktoba 29 na kwenda kupiga kura, na wasikubali kushawishika kuvunja amani ya nchi.

Samia ameyasema hayo Oktoba 1, 2025, wakati wa kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu, katika mji wa Bomang'ombe wilayani Hai Mkoa wa Kilimanjaro, akiwa njiani kuelekea Arusha.

Mgombea huyo, amewahimiza wana CCM na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuinyanyua CCM ili wanaoitazama Tanzania kwa jicho lingine 'waweke heshima'.

"Tukipiga kura kwa wingi, tukiinyanyua CCM kwa wingi, wale wanaoitazama Tanzania kwa jicho lingine wataweka heshima sawasawa," alisema Samia.

Ameongeza: "La pili ninalotaka kuwaambia ndugu zangu msikubali kushawishiwa, mkikubali kushawishiwa tutaharibu amani ya nchi yetu ya Tanzania. Msikubali hata kidogo".

Kulingana na Samia, wale wanaoshawishi kuvunja amani wana mahali pa kukimbilia wao na familia zao.

"Wanaoshawishi wanapo pa kwenda nataka kuwaambia likitokea jambo kidogo tunawakuta Airport (kiwanja cha ndege) pasipoti zao mkononi zina viza tayari wanaondoka, familia zao haziko hapa. Wanachochea kufanya fujo kukikorogeka wakimbie wakaungane na familia zao, sisi tunakwenda wapi? Kwetu ni hapahapa Tanzania, tuilinde nchi yetu kwa wivu mkubwa."

Amewasisitiza vijana wasikubali hilo na wakapige kura na kurejea nyumbani kusubiri matokeo.

"Kwa hiyo nawaomba vijana wangu, watoto wangu, vijana Watanzania msikubali hata kidogo, tokeni kapigeni kura rudi nyumbani subiri matokeo.

Ninawahakikishia usalama na vyombo vya ulinzi vimejipanga vema kutakuwa salama, lakini na ninyi wananchi mtunze usalama," aliongeza.

CHANZO:TRT Afrika Swahili