Kampuni zinazotoa huduma ya usafiri wa majini kati ya Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar, zimesitisha huduma hizo kwa siku ya Oktoba 29, 2025 ili kutoka fursa kwa Watanzania kushiriki zoezi la Uchaguzi Mkuu kikamilifu.
Katika taarifa zao kwa umma, kampuni ya Azam Marine na ile ya Zan Fast Ferries, zimesema kuwa hakutokuwa na safari zozote za boti na meli, kutokana na tukio la kupiga kura siku ya Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
Kulingana na waendeshaji hao wa huduma za usafiri wa majini, safari hizo zitarejea tena Alhamisi ya Oktoba 30.
Wakati huo huo, taarifa kama hizo zimetolewa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Adhrini LATRA ambapo wamiliki wa mabasi Tanzania wametakiwa kusitisha huduma za usafiri siku ya Uchaguzi.
Tanzania itafanya Uchaguzi wake Mkuu Oktoba 29, 2025 ambapo wapigakura 37, 655,559 wamejiandikisha kupiga kura katika majimbo 272.
Kwa mara ya kwanza chama tawala CCM kina mgombea mwanamke. Chama cha CHADEMA hakitoshiriki mchakato huo.
Katika uchaguzi wa Tanzania, matokeo ya Rais hayapingwi kisheria. Hii inamaanisha kwamba uamuzi wa rais unathibitishwa moja kwa moja na haupingiki mahakamani.
Hata hivyo, wagombea waliopoteza katika nafasi za ubunge au udiwani watakuwa na haki ya kupinga matokeo ikiwa wanadhani kulikuwa na kasoro au ukiukaji wa sheria.











