Na Abubakar Famau akiwa Zanzibar
Kura hiyo ambayo inawajumuisha watumishi wa umma pekee kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
Zanzibar, ni kitovu cha utalii nchini Tanzania, na kihistoria inafahamika kila kunapokuwa na uchaguzi nchini humo, hali ya kisiasa hugubikwa na wasiwasi hasa kipindi cha kampeni na baada ya uchaguzi.
Lakini kwa mujibu wa wakazi wa Zanzibar, wanasema siasa za mwaka huu zimekuwa tofauti na miaka iliyopita.
Shaibu Ali Usi, mfanyabiashara katika eneo la Darajani mjini Unguja, ameielezea TRT Afrika jinsi kampeni za mwaka huu zilivyokuwa tofauti na miaka iliyopita.
"Nashukuru sana kwa kampeni za mwaka huu zimekamilika vizuri. Haijawahi kutokea kwa kampeni kufanyika kwa busara. Jumla ya mikutano 73 imefanyika kwa chama tawala na upinzani, hakuna vurugu yoyote iliyotokea," anasema Shaibu.
Nae Hemedi Abdallah Masoud, ambae ni muuza juisi mjini Zanzibar, anaonekana kuwa na mtazamo unaofanana na Shaibu. Yeye anasema, ingawa Afrika bado ina safari ndefu ya demokrasia, lakini ameridhishwa na jinsi kampeni zilivyoendeshwa mwaka huu katika kisiwa hicho, ambacho mara zote kunakuwa na hali ya wasiwasi.
“Kidogo mara hii Zanzibar imeonyesha uchaguzi ni mzuri. Hakuna purukushani za hapa na pale. Hakuna watu kupigwa, wala watu kufukuzwa. Kwa hivyo, tayari tuko katika muelekeo wa kuelekea katika demokrasia," anasema Hemedi.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, Zanzibar ina jumla ya vituo vya kupiga kura 1,772 na wapiga kura 717,557. Kati ya vituo hivyo, ni vituo 50 vilivyotengwa kwa ajili ya kura ya mapema.











