Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), imewasisitiza Waangalizi wa Uchaguzi wa ndani na nje ya nchi kusimamia jukumu lao muhimu la kufuatilia mwenendo wa shughuli za Uchaguzi na kutoa taarifa huru kuhusu namna Uchaguzi unavyotekelezwa bila ya kuingilia kazi za mtu mwengine.
Akizungumza na waangalizi wa ndani na nje ya nchi wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji George alisema kuwa, ZEC imewapa mipaka ambayo inalenga kuhakikisha hawaingilii kazi za wasimamizi wa Uchaguzi, Wagombea au Wapiga Kura.
Kulingana na Jaji Kazi, ni vyema kwa waangalizi hao kutekeleza wajibu wao kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 105 (1) cha Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018, ambacho kinabainisha wajibu kwa waangalizi hao.
Akizungumzia wajibu huo, Jaji Kazi alibainisha kuwa ni pamoja na kuendesha majukumu yao kwa uangalifu, uhuru na malengo lakini pia kuheshimu Sheria za Zanzibar na za Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
“Ndugu waangalizi wa Uchaguzi, tunawaomba nendeni mkazingatie wajibu huu ambao upo kisheria na mutambue kuwa, kupitia kazi yenu wananchi wanapata imani kwamba mchakato wa Uchaguzi ulitekelezwa kwa misingi ya Sheria, Kanuni, Miongozo, Maelekezo, taratibu na uwazi,” alisema.
Alibainisha kuwa ZEC, inatambua nafasi yao kama daraja kati ya wananchi na taasisi za Uchaguzi na kama chombo cha kukuza imani na uwajibikaji.
Hivyo, aliwataka kulinda amani na utulivu katika maeneo yao ya kazi, kuwa mabalozi wa haki na ukweli, wasiwe chanzo cha kuharibu amani ya nchi iliopo, kutoa taarifa kwa wakati, kwa usahihi na kwa uwazi na wawe mfano wa uadilifu unaoweza kuwahamasisha wananchi kuamini katika Uchaguzi wa haki.
Alisema wao ni wadau muhimu katika kufanikisha maendeleo ya Uchaguzi wa Kidemokraia, ukizingatia kuwa ripoti za makundi hayo wanazowasilisha huzisaidia Tume za Uchaguzi kufanya mabadiliko ya Sheria za Uchaguzi na taratibu mbali mbali za uendeshaji ili kuboresha Chaguzi zinazofuata.
Mwenyekiti huyo alisema pia ripoti zao husaidia kubaini mianya mbali mbali na dosari zinazojitokeza katika Uchaguzi kwa vile waangalizi wanakua katika maeneo yote ya Uchaguzi.
“Twendeni sote tukatekeleze majukumu yetu kwa uaminifu, nidhamu, na uzalendo, tuchape kazi kwa pamoja kuhakikisha Uchaguzi unafanyika kwa haki, kwa uwazi na kwa utulivu, tusitoe taarifa zinazoshabikia mirengo ya kisiasa,” alisisitiza.
Akiwasilisha mada ya Uchaguzi Mkuu kwa waangalizi hao, Mkuu wa Kurugenzi ya Mipango, Utumishi na Utawala kutoka ZEC, Saadun Ahmed Khamis, alisema idadi ya wapiga kura ni 717,557 wanaumme 26,443 na wanawake 31,440.
Alisema idadi hiyo ni baada ya kuwafuta Wapiga Kura 4,935 waliopoteza sifa za kuweno katika Daftari kwa mujibu wa kifungu cha 31 (1) cha Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018.
Alibainisha kwamba taratibu zote za Uchaguzi zimekamilika na vifaa vimeshafika katika ngazi ya Wilaya kwa kuanza zoezi ikiwemo ya Kura ya Mapema ambayo itafanyika 28 Oktoba 2025.
Hata hivyo alisema ZEC imeshaandaa maeneo yatakayotumika kufanya majumuisho ya Wapiga Kura kupitia Afisi za Wilaya ambapo kwa Wilaya ya Micheweni ni Skuli ya sekondari Amani Karume, wilaya ya Wete Jamhuri hall na wilaya ya Chake Chake ni ukumbi wa Mwanamashungi.











