Chama cha Alliance For Africa Farmers Party (AAFP) kimejiondoa kwenye mchakato wa uchaguzi wa wabunge na madiwani kwa majimbo ya Arumeru Mashariki na Arumeru Magharibi nchini Tanzania.
Katika taarifa ya chama iliyotolewa na katibu wa chama hicho tawi la Arumeru mkoani Arusha, AAFP imedai kuwa wasimamizi wa uchaguzi wameshindwa kuwapa orodha ya vituo vya kupigia kura katika majimbo ya Arumeru Mashariki na Arumeru Magharibi.
Kulingana na chama hicho, utaratibu huo unakwenda kinyume na kitabu cha maelekezo kwa vyama vya siasa na wagombea, uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2025 Tanzania.
“Kutunyima haki ya kuwa na wakala kwenye vituo vya kupigia kura siku ya kupiga kura kwa kutokutoa taarifa yoyote ya uapishaji na mawakala siku ya saba, kabla ya tarehe ya uchaguzi, kinyume na sheria ya uchaguzi ya mwaka 2024 kifungu 77 (1) na (2),” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Licha ya kuwasilisha malalamiko yao Oktoba 24, AAFP imedai kuwa bado wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo tajwa wameendelea kukaa kimya bila majibu.
“Kwa sababu hizo, wagombea wetu wameamua kujitoa kwa sababu wanaamini hakuna haki itakayotendeka katika uchaguzi huu,” iliongeza sehemu ya taarifa hiyo.











