Ndege ndogo iliyopata ajali siku ya Jumanne nchini Kenya, na kuua watu wote 11 waliokuwa ndani, ilikuwa imebeba watalii wa kigeni kutoka Hungary na Ujerumani.
Shirika la ndege la Mombasa Air Safari limetaja uraia wa abiria waliofariki katika ajali ya ndege Kwale, Pwani ya Kenya. Abiria hao ni wanane, raia kutoka Hungary, wawili ni Wajerumani na rubani wa ndege ambaye ni raia wa Kenya.
“Kwa masikitiko makubwa, hakuna aliyenusurika,” ilisema taarifa ya Mombasa Air Safari. Imeripotiwa kuwa miili ya waathiriwa iliteketea vibaya kiasi cha kutotambulika.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga imeeleza kuwa ajali hiyo ilitokea saa 2:30 asubuhi kwa saa za Kenya (0530 GMT) katika Kaunti ya Kwale, pwani ya Kenya.
Kamanda wa polisi wa eneo hilo, alipokuwa akizungumza kupitia Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC), alisema abiria wote waliokuwa ndani ya ndege walikuwa watalii.
Kituo cha televisheni cha Citizen TV kimeripoti kuwa miili ya waathiriwa iliteketea kiasi cha kutotambulika.
Kwa mujibu wa mamlaka ya usafiri wa anga, ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Diani, eneo la Pwani ya Kenya, kuelekea Kichwa Tembo katika Hifadhi ya Kitaifa ya Maasai Mara.











