Watu wapatao 31 wamethibitishwa kukutwa na maradhi ya Ebola kusini mwa DRC, tangu kuzuka kwa ugonjwa huo mwanzoni wa mwezi Septemba.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Brazzaville, afisa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Patrick Otim, amesema kuwa kumekuwepo na maendeleo katika uchunguzi wa ugonjwa huo, toka ulivyoripotiwa Septemba 4.
“Ni wiki mbili sasa tangu ugonjwa huu uripotiwe. Kufikia sasa, tumethibitisha maambukizi 48,” alisema.
Kulingana na Otim, zaiid ya wagonjwa 15 wanapokea matibabu katika kituo maalumu kilichopo katika mji wa Bulape nchini humo.
Wawili kati ya hao, wameruhusiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus aliwaambia waandishi wa habari jijini Geneva, kuwa shirika hilo limepeleka tani 14 za vifaa vya matibabu, na vile vile kutuma watalaamu wa afya 48 katika kituo maalumu cha kushughulikia maradhi hayo.