Watu wa Shelisheli walipiga kura Jumamosi katika uchaguzi wa kuchagua kiongozi mpya na bunge, huku Rais Wavel Ramkalawan akitafuta muhula wa pili katika nchi ndogo zaidi barani Afrika.
Mpinzani mkuu wa kisiasa wa Ramkalawan, Patrick Herminie wa Chama cha United Seychelles, ni mbunge mkongwe na alikuwa Spika wa Bunge kuanzia mwaka 2007 hadi 2016.
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa 1 asubuhi kwa saa za huko, ishara ya matarajio ya idadi kubwa ya wapiga kura katika taifa hili linalojulikana kwa utalii, ambapo rais huchaguliwa kwa kipindi cha miaka mitano.
Mistari mirefu ya wapiga kura ilionekana katika vituo vingi vya kupigia kura kote nchini Jumamosi. Mamlaka za uchaguzi zilisema vituo vyote vilifunguliwa kwa wakati na upigaji kura ulikuwa ukiendelea vizuri.
Padri Aliyegeuka mwanasiasa
Ramkalawan, padri wa Anglikana ambaye baadaye alijihusisha na siasa, alikua kiongozi wa kwanza wa upinzani tangu mwaka 1976 kushinda chama tawala aliposhinda urais katika jaribio lake la sita mwaka 2020.
Chama tawala cha Linyon Demokratik Seselwa kilifanya kampeni kwa misingi ya kufufua uchumi, maendeleo ya kijamii, na uendelevu wa mazingira.
Iwapo hakuna mgombea atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura, wagombea wawili wa juu wataingia katika duru ya pili. Zaidi ya watu 77,000 wamejiandikisha kupiga kura nchini Shelisheli.
Visiwa 115 vya Shelisheli vilivyo katika Bahari ya Hindi vimekuwa maarufu kwa utalii wa kifahari na mazingira, hali ambayo imeifanya Shelisheli kuwa miongoni mwa nchi tajiri zaidi barani Afrika kwa kipato cha kila mtu, kulingana na Benki ya Dunia.
Mkataba wa Kukodisha Kisiwa
Uchumi pia umechochea kuongezeka kwa tabaka la kati na upinzani dhidi ya chama tawala. Wiki moja kabla ya uchaguzi, wanaharakati waliwasilisha kesi ya kikatiba dhidi ya serikali, wakipinga uamuzi wa hivi karibuni wa kutoa mkataba wa muda mrefu wa sehemu ya Kisiwa cha Assomption, kisiwa kikubwa zaidi nchini, kwa kampuni ya Qatar kwa ajili ya maendeleo ya hoteli ya kifahari.
Mkataba huo, unaojumuisha ujenzi upya wa uwanja wa ndege mdogo ili kuwezesha safari za ndege za kimataifa, umekosolewa sana kwa madai kwamba unawapendelea wawekezaji wa kigeni kuliko ustawi wa muda mrefu wa Shelisheli na uhuru wa ardhi yake.
Kwa eneo lake linalojumuisha takriban kilomita za mraba 390,000, Shelisheli iko katika hatari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa viwango vya bahari, kulingana na Benki ya Dunia na Kikundi cha Maendeleo Endelevu cha Umoja wa Mataifa.
Janga la Dawa za Kulevya
Jambo jingine linalowahusu wapiga kura ni mgogoro unaoongezeka wa dawa za kulevya. Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2017 ilielezea nchi hiyo kama njia kuu ya usafirishaji wa dawa za kulevya. Kulingana na Kielezo cha Uhalifu wa Kimataifa wa Mwaka 2023, taifa hili la visiwa lina viwango vya juu zaidi vya uraibu wa heroin duniani.
Inakadiriwa kuwa watu 6,000 kati ya idadi ya watu 120,000 wa Shelisheli wanatumia dawa hiyo, huku wachambuzi huru wakisema viwango vya uraibu vinakaribia asilimia 10. Wengi wa watu wa nchi hiyo wanaishi katika kisiwa cha Mahé, ambacho ni makao ya mji mkuu Victoria.
Wakosoaji wanasema Ramkalawan ameshindwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti mgogoro wa dawa za kulevya. Mpinzani wake, Herminie, pia alikosolewa kwa kushindwa kupunguza viwango vya uraibu alipokuwa mwenyekiti wa Shirika la Kitaifa la Kuzuia Matumizi ya Dawa za Kulevya na Urekebishaji kati ya mwaka 2017 hadi 2020.