AFRIKA
2 dk kusoma
Julius Malema apatikana na hatia ya kufyatua risasi kwenye mkutano
Julius Malema alishtakiwa kukiuka Sheria ya kumiliki na kudhibiti silaha na huenda akafungwa jela hadi miaka 15.
Julius Malema apatikana na hatia ya kufyatua risasi kwenye mkutano
Chama cha Malema kilipata asilimia 10 ya kura katika uchaguzi mkuu uliopita. / Getty
1 Oktoba 2025

Kiongozi wa upinzani wa Afrika Kusini Julius Malema alipatikana na hatia siku ya Jumatano ya kukiuka sheria ya kumiliki silaha katika tukio la mwaka 2018 ambapo alionekana kwenye video akifyatua risasi katika mkutano wa kisiasa.

Mwanasiasa huyo jasiri, ambaye anaongoza chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters, alishtakiwa kwa kukiuka Sheria ya Kudhibiti Silaha.

Malema huenda akafungwa gerezani hadi miaka 15, lakini kwa kuwa hakuna kifungo cha chini kabisa, hakimu anaweza kumhurumia. Hukumu kuhusu kifungo chake itatolewa Januari 23 mwakani.

Mlinzi wake binafsi wakati huo Adriaan Snyman, ambaye anadaiwa kumpa Malema bunduki hiyo, pia alishtakiwa lakini hakupatikana na hatia. Malema anasema alithibitisha kuwa hakimu alikuwa ni mbaguzi wa rangi, kwa sababu Snyman ni jina la kizungu.

Sherehe za maadhimisho ya chama

Video hiyo ya Malema akifyatua risasi wakati wa maadhimisho ya miaka mitano ya chama chake mkoa wa Eastern Cape ilisambazwa sana 2018. Kundi la wahamasishaji wa Kiafrikaner, Afriforum, liliwasilisha kesi hiyo ya uhalifu dhidi yake.

Katika kujitetea, Malema alidai kuwa bunduki iliyoonekana kwenye video ilikuwa ni ya watoto kuchezea, lakini hili lilikataliwa na hakimu Twanet Olivier.

Malema amewaambia wanaomuunga mkono nje ya Mahakama ya East London kuwa atakata rufaa ya hukumu hiyo hadi katika Mahakama ya Katiba.

Alianzisha chama cha Economic Freedom Fighters, chama cha nne kwa ukubwa nchini Afrika Kusini, ambacho kilipata ushindi wa asilimia 9 katika uchaguzi mkuu wa mwaka uliopita.

CHANZO:TRT Afrika Swahili