Kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola nchini DRC, inazidi kupungua, kulingana na Shirika la Afya Duniani kwa kanda ya Afrika.
Takwimu za hivi karibuni, zinaonesha kuwa, katika kipindi cha kuishia Septemba 28, 2025, ni maambukizi saba tu yaliyoripotiwa, ukilinganisha na 11, yaliyoripotiwa hapo awali.
WHO Afrika, inasema kuwa, hapakuwa na maambukizi yoyote mapya kuanzia Septemba 30, 2025.
Hadi kufikia sasa, zaidi ya watoa huduma za afya 8000 wamepatiwa chanjo, kulingana na WHO Afrika, huku mkazo ukiwekwa kwenye mkakati mpya wa chanjo, utakaolenga kutoa dozi 18,000 katika eneo la Bulape na viunga vyake, kwa lengo la kuzuia kusambaa kwa maambukizi zaidi.
“Dalili hizi zinatia moyo na zinasisitiza umuhimu wa kuongeza jitihada zaidi ili tuokoe maisha,” alisema Mkurugenzi wa WHO Afrika, Dkt. Mohamed Janabi.
“Mwenendo huu unatupa imani ya kumaliza kabisa mlipuko huu.”
Ugonjwa wa Ebola umeua watu 15,000 katika bara la Afrika katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.
Ugonjwa wa Ebola, ambao ni mbaya zaidi nchini DRC, ulitokea kati ya mwaka 2018 na 2020, na kusababisha karibu vifo 2,300 na maabukizi 3,500.