Serikali ya Kenya imewahakikishia raia wake wanaofanya biashara nchini Tanzania kwamba hawataguswa na agizo jipya la leseni lililotolewa hivi karibuni na serikali ya Tanzania.
Kauli hii inafuatia hali ya wasiwasi iliyoibuka awali baada ya chapisho la Leseni za Biashara, la Julai 28, 2025, linalozuia raia wa kigeni kufanya baadhi ya biashara nchini Tanzania.
Kufuatia agizo hilo, Kenya ilifanya majadiliano na serikali ya Tanzania, na kudai kuwa, agizo hilo linaenda kinyume na itifaki ya soko la pamoja la Afrika Mashariki, ambayo inatoa uhakika wa watu kusafiri bila pingamizi, pamoja na kupata huduma, na haki ya kufanya biashara katika nchi wanachama wa Jumuia.
Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, Dkt. Caroline Karugu, ambae ni Katibu Mkuu katika Wizara ya Masuala ya Afrika Mashariki, amesema kuwa kufuatia majadiliano ya pamoja, Tanzania imeihakikishia Kenya kwamba agizo hilo halitawaathiri raia wake.
“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeripoti kwamba, mpaka sasa hakuna biashara ya Mkenya iliyoathirika kufuatia agizo hilo na kuhakikisha kwamba hakuna biashara ya Mkenya itakayoathirika hata kwa siku za baadae,” amesema Dkt Karugu.
Dkt. Karugu amewataka raia wa Kenya waliopo nchini Tanzania kuendelea na shughuli zao bila hofu, na kuwataka kuwasiliana na Ubalozi wa Kenya uliopo nchini humo iwapo kutakuwa na changamoto yoyote.
Wakati huo huo, Kenya imeeleza kuridhishwa na hatua hiyo ya serikali ya Tanzania, na kusema inaonesha utashi wa ushirikiano ndani ya EAC.