AFRIKA
2 dk kusoma
Mkuu wa haki za binadamu UN atoa wito wa kuzuiwa 'ukatili mkubwa zaidi' El Fasher, Sudan
Raia wamezuiwa kutoka Darfur Kaskazini, njaa, mashambulizi yanayoongezeka, anaonya Volker Turk
Mkuu wa haki za binadamu UN atoa wito wa kuzuiwa 'ukatili mkubwa zaidi' El Fasher, Sudan
Volker Turk
2 Oktoba 2025

Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya haki za binadamu ametoa wito wa kuchukuliwa hatua kwa lengo la kuzuia "ukatili mkubwa zaidi, kwa misingi ya kikabila na maafa" huko El Fasher, mji mkuu wa eneo la Kaskazini la Sudan la Darfur, ambapo wapiganaji wa RSF wamezuia watu kutoka kwa zaidi ya siku 500.

"El Fasher iko kwenye hali ya janga kubwa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kuwalinda raia," Volker Turk alisema katika taarifa.

Raia wasiopungua 91 waliuawa kati ya Septemba 19-29 kwenye mashambulizi ya makombora ya RSF, ndege zisizokuwa na rubani, na mashambulizi ya ardhini, kulingana na ofisi ya masuala ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Kumekuwa na mashambulizi ya mara kwa mara katika nyumba, masoko, miskiti, na maeneo ya kupika chakula cha jamii yanayolenga kulazimisha watu kuhama makazi yao, ikiwemo kutoka kwa kambi ya Abu Shouk ambayo watu walioondoka makazi yao wanaishi kwa sasa.

Turk ameonya kuhusu msururu wa ukatili kwa misingi ya kikabila, ikiwemo udhalilishaji wa kingono unaolenga wanawake na wasichana wa jamii ya Zaghawa, kama ilivyoshuhudiwa mwanzoni mwa mashambulizi ya RSF. Alitoa wito wa kuwepo kwa njia salama, na kuruhusu raia wanaotaka kuondoka kwa hiari waondoke, kama vile wazee na wagonjwa, na kutaka kusiwe na vizuizi kwa ajili ya misaada kwa watu.

"Hakuna bidhaa muhimu na bei zinapanda zaidi, raia wako katika hatari ya njaa," amesema, akishtumu vikwazo vya RSF na taarifa za mateso na mauaji kwa kuingiza chakula kimagendo.

"Ukatili uko wazi," mkuu huyo wa masuala ya haki za binadamu alisisitiza na kuongeza: "Haya yanaweza kuepukwa kama wadau wote watachukuwa hatua madhubuti za kuhakikisha sheria ya kimataifa inatekelezwa na maisha ya raia yanalindwa."

CHANZO:AA