Kampuni ya MOFAT kwa kushirikiana na UDART imezindua mabasi mapya yatakayohudumia abiria kutoka Kimara Mwisho kuelekea Gerezani, Kivukoni na Morocco, hayo ni kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo.
Kuwekwa kwa mabasi mapya katika njia hiyo, kunatarajiwa kupunguza kero ya usafiri ambayo imeshuhudiwa katika miezi ya hivi karibuni.
Uzinduzi huu, unakuja saa chache baada ya watu wasiojulikana kuvamia na kuyashambulia baadhi ya mabasi ya Mwendokasi na kuyaharibu, huku kukiwa na malalamiko ya kuzorota kwa huduma hiyo.
Ni katika muendelezo wa matukio hayo ambapo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila alilazimika kukutana na baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam na kujaribu kutuliza hasira zao, huku akiomba msamaha kwa niaba ya serikali.
Awamu ya kwanza ya mabasi hayo ya mwendo kasi imekabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo uchakavu na uchache wa magari, licha ya serikali kuendelea na ujenzi wa awamu nyengine kama ile ya Kariakoo Mbagala na Kariakoo Gongo la Mboto.