Bei za mafuta ya petroli na dizeli zitakazotumika Oktoba mwaka huu nchini Tanzania, zimeendelea kupungua kwa kiwango tofauti ikilinganishwa na zilizokuwepo mwezi uliotangulia, huku upande wa mafuta ya taa ukiendelea kusalia vilevile.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (EWURA), punguzo la gharama za nishati hizo, zinakuwa wakati kukiwa na ongezeko katika soko la dunia kwa asilimia 2.80 kwa mafuta ya petroli, asilimia 3.65 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 3.57 kwa mafuta ya taa.
Kwa jiji la Dar es Salaam, lita moja ya petrol itakuwa inapatikana kwa Dola 1.11 (Shilingi 2,720) kutoka Dola 1.14 (2,807) kama ilivyokuwa kwa mwezi wa Septemba.
Taarifa hiyo, ambayo imesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa EWURA, James Mwainyekule imeongeza kuwa gharama za kubadilisha fedha za kigeni zimepungua kwa asilimia 5.10.
“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko, kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166.
Pia, imevitaka vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.